Thursday, December 6, 2012

JIONEE PICHA ZA OKWI AKISAINI SIMBA MKATABA MPYAAAAA

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, baada ya kusaini jana usiku katika hoteli ya Sheraton mjini hapa.
Okwi alisaini mbele ya Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ambaye ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.
Baada ya kusaini, Okwi alisema; “Nimefurahi kuongeza mkataba na klabu yangu na ninaahidi kuendelea kuitumikia kwa nguvu zangu zote,”alisema Okwi.
Kwa upande wake, Hans Poppe alisema kwamba anaamini kusaini na Okwi sasa kutawakata vilimilimi wapinzani wao, ambao walikuwa wanamuwania mchezaji huyo.
“Sisi tunajua yote yaliyokuwa yakiendelea kwenye Challenge, tunajua wapinzani wetu walimfuata Okwi huku, lakini huyu mchezaji ana mapenzi yeye mwenyewe na Simba SC,”alisema Hans Poppe.
Okwi aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 mjini hapa, alisajiliwa na Simba SC mwaka 2009 akitokea SC Villa ya hapa, baada ya klabu hiyo kumkosa mshambuliaji mwingine Mganda, Brian Umony aliyewahiwa na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Tangu msimu uliopita, Okwi amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Yanga au Azam na akiwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge iliyoanza Novemba 24 na inafikia tamati kesho, ziliibuka habari za klabu hizo kumfuata kumsainisha mjini hapa.
Okwi jana alifunga bao moja kati ya matatu ya Uganda kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, yaliyozima ndoto za Tanzania Bara kurejea nyumbani na Kombe la Challenge.
Kwa matokeo hayo, Uganda itamenyana na majirani zao na wapinzani wao wakubwa, Kenya katika fainali Jumamosi, ambao katika mchezo wa kwanza waliitoa kwa mikwaju ya penalti 4-2 Zanzibar, kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Zanzibar na Bara zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu siku hiyo hiyo ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole.
Hadi mapumziko, Uganda walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Emmanuel Okwi dakika ya 11, baada ta kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa wake, Hamza Muwonge na kufumua shuti kali la umbali wa mita 19, ambalo lilimshinda kipa Juma Kaseja.
Baada ya bao hilo, Okwi aliumia na kutoka nje dakika ya 36 nafasi yake ikichukuliwa na Hamisi Kiiza.
Uganda ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi na kulitia misukosuko lango la Stars kwa takriban dakika 10 mfululizo, lakini baada ya hapo timu hizo zikaanza kushambuliana kwa zamu.
Timu zote zilikuwa zikishambulia kutokea pembeni, lakini Uganda ndio walioonekana kuzalisha mashambulizi ya hatari zaidi.
Kipa na Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alitoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza akilaumiana na mabeki wake kwa kufungwa bao la kutanguliwa.
Kipindi cha pili, Waganda walirudi na moto wao tena na kufanikiwa na kupata bao la pili dakika ya 51, safari hii Robert Ssentongo akimtungua Kaseja, baada ya mabeki wa Stars kudhani ameotea.
Pamoja na kufungwa bao la pili, Stars waliendelea kucheza kwa juhudi, ingawa Waganda waliendelea kutawala mchezo.
Mpira uliotemwa na Juma Kaseja kufuatia shuti la Moses Oloya, ulimkuta Ssentongo dakika ya 71 akaukwamisha nyavuni na kuipatia The Cranes bao la tatu. Kutoka hapo, hali ilikuwa mbaya kwa Stars.
Zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, taa za Uwanja wa Mandela zilizimika, lakini baada ya jitihada za pamoja za FUFA, CECAFA na uongozi wa Uwanja, ziliwaka baada ya dakika saba na mchezo kuendelea hadi filimbi ya mwisho.