Tuesday, April 16, 2013

BILIONEA: BABU SAMBEKE KUAGWA KESHO NYUMBANI KWAKE NJIRO ARUSHA ..

 
DSCF8826
Enzi ya uhai wake Babu Sambeke akiwa na moja ya ndege yake

DSCF8777
Hii ndiyo ndege iliyokatisha maisha ya bilionea maarufu Babu Sambeke iliyodondoka karibu na uwanja wa ndege wa kisongo Arusha

DSCF8823
Msemaji wa familia Dk.Richard Masika akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu themi njiro kuhusu taratibu za mazishi

 

DSCF8825

Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu

DSCF8824

Moja ya choo cha ndani kilichopo katika jumba la kifahari la Bilionea Babu Sambeke

 

**********

Mwili wa Bilionea maarufu wa Mkoani Arusha na mjini Moshi,Ernest Sambeke unataraji kuagwa rasmi Njiro kesho jijini Arusha kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.


Heshima za mwisho zinatarajiwa kuanza rasmi majira ya saa 7;00 mchana ambapo watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa hapa nchini wanataraji kutoa heshima zao za mwisho nyumbani kwa marehemu Njiro jijini Arusha.


Marehemu Sambeke alifariki juzi katika ajali ya ndege iliyoanguka katika eneo la Kisongo jijini Arusha ambapo taarifa za wali zilisema kuwa alipata majeraha katika eneo la kichwa na kifuani na kupelekea kupoteza maisha.

 
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu jana msemaji wa familia hiyo,Dk Richard Masika alisema kuwa mwili wa marehemu utaagwa kesho na kisha kusafirishwa kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuzikwa.

 
Alisema kuwa kabla ya mazishi ya marehemu kutakuwa na misa ya kumuombea itakayofanyika katika kanisa la Roman Catholic(RC) majira ya saa 8;00 lililopo Karanga wilayani Moshi na kisha kuzikwa nyumbani kwake eneo la Karanga majira ya saa 10.00.

 
Masika alisema kuwa marehemu alizaliwa Mwezi juni mwaka 1964 mkoani Kilimanjaro na ameacha mke mmoja aliyetambulika kwa jina la Marcelina Sambeke pamoja na watoto watatu ambao ni Jamal,Sian pamoja Getrude.


Hatahivyo,alisema kuwa mali alizokuwa nazo marehemu zikiwemo fedha wakati akipatwa na mauti tayari zimepatikana ambapo jeshi la polisi mkoani Arusha limeziwasilisha mbele ya familia ya marehemu.


Bila kutaja mali zipi na fedha kiasi gani alisema kuwa tayari wamepokea taarifa ya kifo cha marehemu kuwa alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata ambayo ni upande wa kifua na kichwa.

Wakati huo huo Masika alishindwa kuthibitisha taarifa zinazodai kuwa ndege aliyofia marehemu ilikuwa ikimilikiwa na wakili maarufu aliyefariki na kuzikwa hivi karibuni nchini Kenya,Nyaga Mawalla huku akisema kuwa hana ushahidi wa kutosha.


Ameongeza kuwa, marehemu alikuwa akimiliki ndege mbili wakati wa uhai wake huku akisema kuwa atakumbukwa kwa ucheshi,upendo pamoja na ushirikiano wake.

 

"Marehemu alikuwa akijihusisha na suala la ujasiriamali huku akimiliki ndege mbili ndogo", alisema Msemaji huyo.