Thursday, May 23, 2013

LWAKATARE WA CHADEMA AENDELEA KUSOTA LUMANDE

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amewasilisha ombi katika Mahakama ya Rufaa nchini, akiomba itengue uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wa kumfutia mashitaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Dk. Feleshi aliwasilisha ombi hilo juzi kwa njia ya maandishi, ambapo katika maombi yake anaiomba mahakama hiyo iitishe mwenendo wa shauri lililotolewa uamuzi huo na Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrence Kaduri Mei 8, mwaka huu na kuupitia upya na ifute uamuzi huo kwa kuwa una makosa kisheria.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Dk. Feleshi anadai Mahakama Kuu haikuombwa kumfutia mashitaka Lwakatare kama Jaji Kaduri alivyotoa uamuzi huo, bali aliiomba mahakama iitishe majalada ya kesi ya msingi iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na 20 mwaka huu.

“Kwa kuwa Ofisi ya DPP ipo kwa ajili ya kusimamia utawala wa sheria, haijaridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu uliomfutia mashitaka matatu Lwakatare, hivyo tunaiomba mahakama hii iitishe mwenendo wa kesi ulioamuliwa, kwani tunaamini kisheria jaji alikosea kutoa uamuzi ule, kwani Lwakatare hakuwa ameomba afutiwe mashitaka yanayomkabili,” alidai Dk. Feleshi.

Hata hivyo hadi jana mchana uongozi wa Mahakama ya Rufaa ulikuwa bado haujapanga majaji wa kusikiliza ombi hilo.

No comments: