Monday, May 13, 2013

MATOKEO YA FORM 6 HAYOTATOKA MPAKA MATOKEO MAPYA YA FORM 4 YATANGAZWE:: MULUGO


      Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotarajiwa kutangazwa mwezi huu yatachelewa ili kutoa nafasi kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kurekebisha matokeo mabaya ya mitihani kidato cha nne ya mwaka jana yaliyofutwa na serikali mwezi huu.
        
         Matokeo ya kidato cha sita ambayo huwa yanatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei mpaka sasa hayajatolewa na kwamba hayatatangazwa mpaka matokeo mapya ya kidato cha nne yatakaporekebishwa rasmi.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Naibu Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi Philipo Mulugo alisema ingawa wakati huu ndio unaopaswa yatangazwe matokeo ya kidato cha sita haitafanyika hivyo hadi yatangazwe matokeo mapya ya kidato cha nne baada ya kufutwa.
http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Philipo%20Mulugo.jpg

Hata hivyo, akasema huenda yakatolewa pamoja au yakafuata wakati mwingine lakini mara baada ya kukamilisha kazi ya kurejea na kusahihisha matokeo ya kidato cha nne.


"Siyo kwamba yamechelewa kwani muda wa kujiunga na chuo ni Septemba hivyo haitawaathiri kwa hilo," alisema Mulugo.
 
      Kuhusu hatma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao wapo mashuleni wanaendelea na masomo ya kidato cha sita, alisema kama kutakuwa na wanafunzi ambao wapo madarasani shule zilizowasajili zitakuwa hazijafuata mfumo wa elimu unavyoelekeza.
 
     Alifafanua kuwa mfumo wa elimu kwa kidato cha nne ulibadilishwa na kwamba endapo mwanafunzi akifaulu anatakiwa kujiunga rasmi kidato cha sita Julai na si vinginevyo.
 
        Alisema licha ya ucheleweshaji wa matokeo hali hiyo haikuwaathiri wanafunzi hao kwa kuwa ratiba ya kwenda masomoni haijaanza kwa mujibu wa kalenda ya shule ya serikali.
 
    Serikali ilifuta matokeo ya kidato cha nne ya 2012 na kuiagiza Necta kuyaandaa upya kwa kutumia utaratibu wa usahihishaji na upangaji madaraja uliotumiwa mwaka 2011
 
     Taarifa ilisema mfumo uliotumika mwaka jana na kusababisha wanafunzi kushindwa vibaya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
 
       Matokeo hayo yaliyotangazwa mwezi Februari mwaka huu yalionyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi walishindwa mtihani.

No comments: