Wednesday, July 17, 2013

RAISI JK AMTAKA RAISI OMAR BASHIRI WA SUDANI KUWACHUKULIA HATUA KALI WOTE WALIOHUSIKA NA VIFO VYA WANAJESHI WA TANZANIA




Rais Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Rais wa Sudan Omar Hassan el Bashir hivi karibuni wakati wa Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika jijini Addis Ababa Ethiopia. (PICHA NA MAKTABA YETU).
 ---

             Rais Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Sudan Mheshimiwa Omar Bashir kufuatia kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika jimbo la Darfur na kumtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.

           Katika mazungumzo yao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi kuwasaka hadi kuwakamata wale wote waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

       Rais Bashir amemueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini kuwa waliohusika ni wahalifu na hivyo kuahidi kuwa lazima
watasakwa hadi kukamatwa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Rais Bashir amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha ambapo wanajeshi wa Tanzania wameenda nchini Sudan kulinda Amani na Usalama wa wananchi wa Sudan.

           Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Bw. Ban Ki Moon alimpigia Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha ambao umewatokea wa Tanzania hao wakati wakiwa katika kutekeleza jukumu lao la kulinda amani nchini Sudan.

             Hadi sasa hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo ingawaje kumekua na kutupiana lawama baina ya vikundi vya kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur.

              Mapigano baina ya vikundi vya kikabila na koo mbalimbali zimesababisha mapigano na uvunjifu mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa miaka 10 sasa, na mara nyingi mapigano na tofauti zao hizo zimesababisha vifo na uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni pia.


No comments: