Wednesday, July 10, 2013

SIMBA YAANZA KUIVA YATEMBEZA KIPIGO KWA RHINO FC




SIMBA SC imemaliza vyema ziara yake ya mkoani Katavi jioni ya leo kwa kuifunga timu ya kombaini ya Katavi mabao 2-1 kwenye Uwanja wa wazi wa Katavi mkoani humo. 

          Simba SC, ambayo ipo Katavi kwa mwaliko wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mchezo wake wa kwanza iliibamiza Rhino FC ya Tabora iliyopanda Ligi Kuu msimu huu mabao 3-1.

           Na leo mabao ya mshambuliaji aliye katika majaribio kutoka Al Ahly Shandi ya Sudan Kusini, Kun James kipindi cha kwanza na beki Mganda, Samuel Ssenkoom yamewapa ushindi mwingine Wekundu hao wa Msimbazi. Jumapili, mabao ya Simba yalifungwa na Edward Chirstopher mawili na moja Nahodha mpya, Nassor Masoud ‘Chollo’.
Hataki mechi Dar; King Kibaden anataka Simba SC icheza Dar es Salaam ikiiva vizuri

         Baada ya mechi hiyo, kocha Mkuu wa Simba SC, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ anataka timu iende mikoa ya kanda ya Ziwa kucheza mechi nyingine za kirafiki.

       Wakati huo huo, George Wakuganda ameialika timu ya U.R.A. ya Uganda kwa ajili ya kucheza na Simba SC Julai 20, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na japokuwa amekwishafanya mazungumzo na uongozi wa klabu, lakini Kibadeni hayuko tayari kuianika timu yake Dar es Salaam kwa sasa.HABARI24 inafahamu Kibadeni amewaambia viongozi kwamba, anataka ahakikishe timu yake imeiva kiasi cha kutosha ndipo airuhusu kucheza Dar es Salaam, vinginevyo mashabiki wa timu hiyo watalazimika kuisubiri hadi wakati mwa tamasha la Simba Day, Agosti 8, mwaka huu.

              Hata Kamati ya Utendaji ya Simba inaunga mkono wazo la Kibadeni, ikiamini pia kwamba timu yao ikicheza mechi yoyote kabla ya Agosti 8, itawaathiri kimapato katika Simba Day- hivyo wanataka watengeneze hamu kubwa ya mashabiki kwa timu yao.

No comments: