KUMEKUCHA--HII NDIYO TAARIFA YA MBUNGE WA CHADEMA WENJE KUHUSU MGOGORO WA CHINI CHINI KATI YA TANZANIA NA RWANDA        
           Kwa siku kadhaa sasa baadhi ya vyombo vya habari nchini, vikinukuu Gazeti la Serikali ya Rwanda la ‘News Of Rwanda’ vimekuwa vikiandika habari ambazo zinaashiria kuwepo kwa dalili za kurudi tena kwa hali tete ya kiuhusiano kati Tanzania na Rwanda.
          
        Chanzo cha habari cha baadhi ya vyombo hivyo vya hapa nyumbani ni habari iliyoandikwa na Gazeti la Serikali ya Rwanda liitwalo Nes of Rwanda ambalo limekakaririwa likiripoti kwa kutuhumu kuwa hivi karibuni Tanzania ilikuwa mwenyeji wa viongozi wa chama cha upinzani huko Rwanda cha RNC na kikundi cha waasi dhidi ya Serikali ya Rwanda cha FDLR.
ENDELEA--------


         
           Ripoti hizo zimedai kuwa waasisi wawili wa chama cha Rwanda National Congress (RNC) akiwepo Dr.Theogene Rudasingwa walikutana Dar Es Salaam pamoja na makamanda wa ngazi ya juu wa kikundi cha waasi cha FDLR.
      
         Ilidaiwa kuwa Mratibu wa chama cha RNC Dr.Theogene Rudasingwa na mshauri wa chama hicho Condo Gervais walikiwakilisha chama hicho cha upinzani huku kikundi cha waasi cha FDLR kikiwakilishwa na Katibu mkuu Mtendaji Luteni Kanali Wilson Rategeka na Kanali Hamadi ambaye ni kamanda wa operesheni
        
       Gazeti hilo kupitia habari zake liliripoti kuwa maofisa wa FDLR wanasafiri kwa kutumia hati za kusafiria (paspoti) za Tanzania.
Wiki moja kabla ya ripoti hiyo, gazeti hilo hilo la Serikali ya Rwanda, liliandika habari kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda Faustin Twagiramungu alikua nchini Tanzania tangu Januari 19,2014 kabla ya kusafiri kuelekea jijini Lyon, Ufaransa ambako alihudhuria mkutano wa wajumbe wa chama chake cha upinzani cha RDI (Rwanda RWIZA).
        
    Gazeti hilo lilimnukuu Twagiramungu akizungumza mbele ya kikao hicho kuwa alikuwa nchini Tanzania kwa kile alichokiita ni “Malengo Mahsusi”
      
         Aidha gazeti hilo liliendelea kueleza kuwa tarehe 20 Decemba, 2013 Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi walisafiri kwa kutumia hati za kusafiria za Tanzania kuelekea nchini Msumbiji kwa mazungumzo na watu wanaodaiwa kuwa ni mamluki wa chama cha RNC.

         Ubalozi wa Tanzania Rwanda ulikanusha tuhuma hizo kwa misingi ya kuwa idara ya uhamiaji ya Tanzania haina kumbukumbu juu ya watu hao kuingia Tanzania na pia Rais Kikwete hakuwa nchini Tanzania Tarehe 23/01/2014, hivyo madai kuwa alikutana na viongozi wa vyama hivyo au kikundi cha waasi kwa nafasi yake, si kweli.

       Pamoja na Serikali kupitia Ubalozi etu nchini Rwanda kukanusha, kupitia taarifa hii kwa umma, tunaitaka serikali yetu kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na;

1.    Kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mtiririko wa tuhuma hizo, hasa zile zinazohusu matumizi ya pasi za kusafiria ili kujiridhisha pasi na shaka kuwa jina la nchi yetu halitumiki vibaya kuweza kuhatarisha uhusiano wa kidiplomasia na majirani zetu tena ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

2.    Kutokana na ukweli kuwa Idara ya Uhamijai ni moja ya taasisi zenye uozo mkubwa unaoendana na vitendo vya rushwa, ni vyema serikali ikajiridhisha na kuridhisha Watanzania kwa hakika kwamba hakuna  maofisa wa juu wa serikali ya Tanzania kwa maelekezo au sababu zao binafsi walishiriki katika utoaji wa hati za kusafiria kwa watu hao wasiokuwa raia wa Tanzania katika hali inayotia shakani uhusiano wetu na nchi jirani..

        Matumizi mabaya ya hati ya kusafiria kama utambulisho wetu kimataifa ni makosa makubwa yanayokiuka mikataba ya kidiplomasia, sheria za kimataifa na yanayochafua sura ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa endapo hati hizo zitaangukia mikononi mwa watu wabaya kama ilivyotokea miaka miwili iliyopita pale ambapo utambulisho wa taifa letu (bendera) ulipotumika katika meli za nchi moja kukwepa vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

3.    Tunataka Bunge la Tanzania kupitia Kamati ya Mambo ya Nje, kuunda kamati ndogo ambayo italifanyia kazi suala hili la uhusiano wa nchi yetu na Rwanda ambao umekuwa ukionesha hali ya kulega lega kutokana na chokochoko za maneno kutoka kila upande.

4.    Aidha tunataka pia kujua msimamo wa Serikali ya Tanzania juu ya kauli za Twagiramungu ambaye amenukuliwa akisema mbele ya kikao cha chama chake kuwa alikuwa nchini kwa malengo mahsusi! Malengo hayo ni yapi?

Tangu taarifa hizo zilipochapishwa, Serikali ya Rwanda imekaa kimya.Wizara ya mambo ya nje haikuchukua hatua yoyote hata kumuhoji balozi wa Rwanda nchini Tanzania kutoa msimamo wa serikali yake .Heshima ya Tanzania kimataifa imewekwa rehani kwa tuhuma hizi nzito hasa kipindi hiki ambacho uhusiano wa Tanzania na Rwanda ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki umeonekana ukilega lega

Mkataba wa Umoja wa Afrika (AU Chartter) –Ibara ya 3(b) umeainisha kuwa kila nchi mwanachama zinatakiwa kuheshimu uhuru na mipaka ya nchi nyingine bila kuingilia mambo ya ndani isipokua pale ambapo Umoja wa Afrika unapoona haja ya kufanya hivyo kupititia Kikao cha Mkutano mkuu wa Afrika au Ikiwa kuna janga kubwa linalohusisha mauaji ya kimbari au uhalifu dhidi ya binadamu kwa mujibu wa Ibara ya 4(a), (b), (f) ya kanuni za uendeshaji wa umoja wa Afrika,au nchi mwanachama inapoomba msaada

       Sasa habari hizi kuwa Tanzania inaingilia maswala ya ndani ya nchi nyingine ambayo ni mwanachama mwenza ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika ni hatarishi kwa mahusiano ya kidiplomasia ambazo hazitakiwi kujibiwa kwa hoja nyepesi kuwa Rais hakuwepo nchini muda huo bali tulitarajia serikali ingeenda mbali zaidi katika kufanya uchunguzi wake na pia kuomba ufafanuzi wa misingi ya tuhuma hizo kutoka serikali ya Rwanda kwa kuwa chombo kilichoripoti habari hiyo ni chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali ya Rwanda.

Hivi karibuni iliripotiwa kuwa chama cha RDI kimetangaza kuwa kipo tayari kuuondoa utawala wa Kigali madarakani kwa kutumia nguvu jambo ambalo ni kinyume na  na ibara ya 4 ya mkataba wa uanzishwaji wa umoja wa Afrika(AU) ambayo imekataza kutoitambua njia ya kubadili utawala kinyume na taratibu za kikatiba na hivyo kuzuia serikali zilizoingia madarakani kwa njia hiyo kushiriki shughuli za umoja huo.

Itakuwa ni jambo la fedheha kwa nchi kama Tanzania kuingizwa katika mambo yanayozua mgogoro na hata kupelekea kukwamisha malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata Umoja wa Afrika ambao tulikubali kuhakikisha malengo ya utengamano kupitia taasisi hizi za kimataifa yanatimia.

Kwa upande wa FDLR ikumbukwe kuwa si chama cha siasa bali kikundi cha waasi ambacho Serikali ya Kigali imekuwa ikikituhumu kwa kufanya mauaji ya kimbari (genocide) kule Rwanda. Ni fedheha kwa serikali yetu kutochukulia kwa uzito suala hili linaloweza kutoa taswira kuwa Tanzania ina ushirika na vikundi vinavyokumbatia itikadi inayopigwa vita na jumuiya ya kimataifa.

Mbali na serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo, serikali ya Tanzania ilitakiwa kumuhoji Balozi wa Rwanda juu ya msimamo wa serikali yake kutokana na habari iliyoandikwa na chombo hicho ili kuboresha mahusiano mema kati ya Tanzania na Rwanda na pia kwa maslahi mapana ya utengamano wa jumuiya ya Afrika Mashariki

Tunatoa rai kwa Kamati ya bunge ya Mambo ya Nje na kamati ya ulinzi zichunguze suala hili linalohatarisha mahusiano ya nchi zetu mbili kwa kuwa sio mara ya kwanza kwa mahusaiano haya kutetereka

Nchi hizi mbili zina historia iliyotukuka kimahusiano. Kwa upande wetu tuliunga mkono jitihada za Rais Kikwete kulitangazia Bunge juu ya dhamira yake ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na majirani zetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tunaendelea kutoa wito kwa serikali kuchukua hatua za kidiplomasia na kuzingatia misingi y a sheria za kimataifa ili kulinda hadhi ya taifa letu kimataifa na pia kusimamia misingi ya sera zetu za mambo ya nje.

Imetolewa leo Februari 4, 2014 na;
Ezekia Wenje (MB)
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje-CHADEMA

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.