Sunday, July 13, 2014

KIINGILIO MECHI YA SERENGETI BOYS HIKI HAPA

Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Afrika Kusini (Amajimbos) itachezwa kwa kiingilio cha sh. 2,000.
Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam ndiyo utakaokuwa mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 9 kamili alasiri.

Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Shelisheli. Mwamuzi wa kati ni Allister Barra wakati wasaidizi wake ni Gerard Pool na Jean Joseph Felix Ernest wakati mezani atakuwa Nelson Emile Fred.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Andriamiasasoa Doda Nirimboavonjy kutoka Madagascar.

Kikosi cha Serengeti Boys chini ya kocha Hababuu Ali Omari kipo kambini kwa zaidi ya wiki mbili sasa kikijiandaa kwa mechi hiyo. Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 nchini Afrika Kusini.

Wakati huo huo, Alfred Kishongole Rwiza wa Tanzania ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya michuano hiyo ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Rwanda na Uganda.

Mechi hiyo itachezwa nchini Rwanda kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu. Waamuzi wa mechi hiyo watatoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)


No comments: