Sunday, July 20, 2014

STARS HOI TAIFA-TZ 2---MSUMBIJI 2

Mbwana Samatta katika eneo la tukio akisababisha penati.
Mbwana Samatta katika eneo la tukio akisababisha penati.
Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imelazimishwa sare ya magoli 2-2 na Msumbiji katika mechi ambayo walikuwa katika nafasi ya kushinda – ni katika hatua za awali za mechi za kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yatakayofanyika Morocco, 2015.

Baada ya kutangulia kufungwa katika dakika ya 47 kwa penalti iliyovushwa mstari na Elias Pelembe kutokana na Kevin Yondan kucheza rafu kwenye eneo la hatari, Taifa Stars ilisawazisha dakika ya 65 mfungaji alikuwa Khamis Mcha akimalizia kazi nzuri ya Thomas Ulimwengu.
Mchezaji huyo wa Azam, akaingia tena katika orodha ya wafungaji katika dakika ya 71 kwa penalti, baada ya mabeki wa Mambas kumchezea rafu Mbwana Samatta kwenye eneo la hatari.Mpaka dakika za mwisho ikaonekana kama Stars wanashinda mechi hiyo muhimu.
Hata hivyo Msumbiji walizinduka na kufanya shambulizi la uhakika ambalo lilizaa goli kunako dakika ya 87 kupitia kwa Isaac Carvalho aliyeingia kama mchezaji wa akiba.
Matokeo hayo yameiweka pabaya Taifa Stars ambayo itajitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele, au sare ya kuanzia mabao 3-3, wakati wenyeji wanaweza kunufaika na sare ya 1-1 au 0-0. Ikiwa 2-2 tena, mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Katika mchezo huo, uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo, mabao ya Stars inayofundishwa na Mholanzi Mart Nooij yalifungwa na kiungo wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa.

No comments: