Saturday, September 20, 2014

YEMETIMIA--LIGI KUU TANZANIA BARA IMERUDI TENA,SOMA ILIKOTOKEA NA HISTORIA YAKE HAPA


Makala hii imeandikwa Na Mahmoud Zubeiry, 


HATIMAYE michuano mikubwa kabisa ya soka nchini, ijulikanayo kama Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inarejea tena kwa mara ya 51 tangu ilipoanzishwa mwaka 1965 kwa wigo finyu na hali dunia kabisa, ikishirikisha klabu za Dar es Salaam pekee.

Naam, msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), unatarajiwa kuanza Jumamosi ya leo, timu 14 zikijitupa dimbani kuwania pointi za mwanzoni, katika mbio za kusaka ubingwa wa ligi, unaoshikiliwa na Wana Jangwani, Yanga SC. 
Historia ya ligi hiyo inaanzia mwaka 1929 ilipoanzishwa kifukara, tu kwa sababu ya mapenzi ya watu na soka wakaamua kuungana na kuanzisha michuano ya kutafuta bingwa, ingawa ni timu za Dar es Salaam pekee zilizokuwa zikishiriki wakati huo.



Kufika mwaka 1965, ilianzishwa michuano ya Klabu Bingwa Tanzania, ambayo ilikuwa inaanzia ngazi ya Wilaya, ikichezwa kwa mtindo wa mtoano, ingawa pia katika miaka miwili ya mwanzoni, timu za Dar es Salaama pekee ndizo zilizoshiriki.

Katika mfumo huo, bingwa wa kwanza ilikuwa ni klabu ya Sunderland ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo ilifanikiwa kutetea ubingwa wake msimu uliofuata, kabla ya kuutema kwa Cosmopolitan ya Dar es Salaam pia mwaka 1967.

Lakini wakati wote huo, bado Tanzania ilikuwa haijawa mwanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hivyo Sunderland hawakuwahi kucheza michuano ya Afrika. Cosmo ingekuwa ya kwanza kucheza Klabu Bingwa Afrika mwaka 1968 kama isingejitoa, lakini kwa kujitoa kwao, Yanga ilifungua historia ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika mwaka 1969, baada ya kutwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya kwanza mwaka 1968, kabla ya kuutetea mara nne mfululizo, katika miaka ya 1969, 1970, 1971 na 1972. Baada ya hapo, Sunderland ikiwa tayari imebadili jina na kuitwa 

Simba kurejesha taji lake mwaka 1973.
Simba ilishindwa kuutetea ubingwa wake msimu uliofuata mwaka 1974 baada ya kupokonywa na Yanga katika fainali ya kihistoria iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kwa kuchapwa mabao 2-1.  

Mwaka 1975 Yanga iliutema ubingwa huo kwa Mseto SC ya Morogoro, iliyoweka historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa nchi.

Lakini Mseto ilishindwa kuteteqa taji hilo, ikapokonywa na Simba msimu uliofuata- na Wekundu wa Msimbazi walifanikiwa kutetea ubingwa huo kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.

Siri ya kutawala kwa Simba kwenye ligi hiyo kwa miaka yote hiyo ni kuyumba kwa Yanga baada ya kukumbwa na mgogoro mkubwa 1976, uliosababisha kukimbiwa na wachezaji wote nyota, hivyo kuanza upya kabisa kuunda timu. 

Ni ndani ya kipindi hicho Simba iliweza kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 5-0 na Yanga mwaka 1968, wakati nayo ilipowatandika watani wao hao wa jadi 6-0 mwaka 1977.  
Juni 1, mwaka 1968 Yanga iliigaragaza Simba 5-0, mabao yake yakitiwa kimiani na Maulid Dilunga (sasa marehemu) katika dakika za 18 kwa njia ya penalti na 43, wakati mengine yalitiwa kimiani na Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89 kabla ya Kitwana Manara kupachika la kuhitimisha karamu ya mabao dakika ya 86.

Julai 19, mwaka 1977 Simba nayo ililipa kisasi kwa kuibugiza Yanga mabao 6-0, wafungaji wakiwa ni Abdallah 'King' Kibadeni aliyetikisa nyavu mara tatu katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mengine yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73 na Selemani Sanga wa Yanga alijifunga dakika ya 20.

Kufika mwaka 1981, tayari Yanga ilikuwa imara tena na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara ingawa msimu uliofuata iliutema kwa Pan African. 
Kuanzia mwaka 1982, mfumo wa Ligi ya Tanzania ulibadilishwa na kukawa na ligi tatu, kwanza ni Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza visiwani Zanzibar na Ligi Kuu ya Muungano.

Yaani baada ya kupatikana washindi wawili wa juu wa kila ligi, Bara na Visiwani, walikutana kwenye Ligi Kuu ya Muungano, kutafuta bingwa wa Tanzania na washindi wake.
Wakati huo, bingwa wa Ligi ya Muungano alikwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili alicheza Kombe la Washindi.

Baadaye timu ziliongezwa na kuwa tatu kila upande katika Ligi ya Muungano.

Mwaka 1983, Yanga ilirejesha taji hilo kwenye himaya yake, ingawa msimu uliofuata ililitema tena kwa Simba.  Kwa ujumla muongo mzima wa 1980, taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara lilikuwa la kukoponyana, kwani Simba nayo mwaka 1985 ilipokonywa taji hilo na Yanga, ambayo nayo ililitema kwa timu mpya katika Ligi Kuu msimu wa 1986, Tukuyu Stars ya Mbeya.
Tukuyu nayo iliwarejeshea Yanga taji lao mwaka 1987, wakati mwaka 1988 Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga ilijiingiza katika orodha ya timu zilizowahi kutwaa taji hilo. 

Mwaka 1989, Yanga ilifunga orodha ya mabingwa ya mabingwa wa muongo huo kwa kutwaa tena ubingwa wa Bara.
Simba iliibuka mwaka 1990 na kutwaa ubingwa huo, ikitoka kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita. 

Kupokonyana taji kuliendelea hata kwenye muongo wa 1990, kwani Simba iliutema ubingwa huo kwa Yanga mwaka 1991.
Yanga iliutetea ubingwa huo mara mbili mfululizo katika miaka ya 1992 na 1993, kabla ya kupokonywa na Simba mwaka 1994. 

Simba ilifanikiwa kuutetea mara moja 1995.
Mwaka 1996 ndipo Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilipozaliwa rasmi chini ya udhamini wa Bia ya Safari Lager, bia inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na ikijulikana kama Safari Lager Premier League, Yanga ndiyo iliyokuwa bingwa wake wa kwanza. Yanga iliutetea ubingwa huo kwa miaka miwili mfululizo 1997 na 1998. 

Mwaka 1999, Yanga ikiwa tayari imetwaa ubingwa kwa matokeo ya uwanjani, aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, alitengua matokeo hayo kwa kuiongezea Mtibwa Sugar pointi za mezani, hivyo kuipiku Yanga. Hatimaye Mtibwa ilipata ubingwa wa mezani.

Mtibwa ilifanikiwa kutetea ubingwa mwaka 2000, kabla ya kupokonywa na Simba msimu uliofuata, ingawa Yanga iliibuka mwaka 2002 na kuutwaa tena ubingwa huo.

Mwaka 2003 Simba iliyokuwa kali zaidi ilifanikiwa kuutwaa tena ubingwa huo na kuutetea mwaka 2004 kabla ya kupokonywa na Yanga 2005 ambao waliutetea 2006. Mwaka 2007, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya mabadiliko ya kalenda yake, ikitaka Ligi yake iendane na ligi za Ulaya, hivyo ikaamua kuchezesha ligi ndogo ya mpito kumpata bingwa na mwakilishi wa Kombe la Shirikisho, kabla ya Ligi Kuu kuanza rasmi Agosti.

Simba iliibuka bingwa wa ligi hiyo, baada ya kuifunga Yanga kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kufuatia sare ya 1-1.
Lakini msimu uliofuata ikiwa chini ya Profesa wa Kiserbia, Dusan Savo Kondic, Yanga ilifanikiwa kuurejesha ubingwa wake msimu wa 2008 na kutetea msimu uliofuata ikiwa chini ya kocha huyo, ambaye hata hivyo msimu uliopita alitupiwa virago katia mzunguko wa kwanza tu wa ligi na nafasi yake kuchukuliwa na Mserbia mwenzake, Kostadin Bozidar Papic, ambaye alishindwa kubakisha taji Jangwani, baada ya Simba kuchukua kwa kishindo.

Simba ilishinda mechi zote ikiwemo mbili dhidi ya watani wa jadi, Yanga na kutoa sare mbili tu dhidi ya Kagera Sugar Bukoba na African Lyon Dar es Salaam, hivyo kutwaa ubingwa kwa mbwembwe za aina yake na kufanikiwa kuutetea 2010.
Mwaka 2011 taji lilikwenda Jangwani yalipo maskani ya Yanga SC, kabla ya 2012 kuhamia Msimbazi kwa Simba SC. Mwaka 2013  Yanga walirudisha taji lao na Mei mwaka huu, Azam FC iliweka historia ya kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa ligi hiyo.

Wakati Ligi Kuu ikizipoteza timu za Ashanti United, JKT Oljoro na Rhino Rangers zilizoterenka daraja msimu uliopita, msimu huu zimeibuka timu nyingine ambazo ni Polisi ya Morogoro, Stand United ya Shinyanga na Ndanda FC ya Mtwara.

Polisi imewahi kucheza Ligi Kuu mara kadhaa na kuteremka kuanzia muongo uliopita, wakati Ndanda na Stand zinapanda kwa mara ya kwanza. 

Pazia la kuashiria kufunguliwa kwa msimu uliopita lilipenuliwa rasmi kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga SC na Azam Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga SC walishinda 3-0.

Mechi za ufunguzi leo zinatarajiwa kuwa kati ya mabingwa watetezi, Azam FC na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, wakati washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kilio kikubwa cha wapenzi wa soka nchini ni kuhusu waamuzi, hawa wamekuwa wakilalamikiwa sana kwa kuharibu ladha ya ligi, kutokana na kuzibeba baaadhi ya timu.

Kuna kashfa ya rushwa kwa waamuzi Ligi Kuu, kuna timu zinatuhumiwa kuhonga marefa ili zisaidiwe kushinda, hili bado TFF haijatoka na jibu sahihi, lakini kweli waamuzi wanavurunda.   Pamoja na yote, matarajio yanabaki pale pale, itakuwa ligi yenye ushindani mkubwa na ubingwa utapatikana kwa jasho haswa. 

Neema zaidi imeletwa na kampuni ya Azam Media Limited iliyonunua haki za matangazo ya Televisheni msimu uliopita, ambayo inafanya kila klabu ipatiwe zaidi ya Sh. Milioni 100 kwa msimu. Wazi, fedha hizi zitasaidia sana klabu, pamoja na zile za wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom maana yake timu zitapunguza matatizo ya kifedha kwa kiasi kikubwa. 

Mara ya mwisho taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara lilitoka nje ya Dar es Salaam mwaka 2000, walipolibeba Mtibwa Sugar ya Morogoro, lakini tangu hapo timu tatu tu za Dar es Salaam zimepokezana taji, hilo Simba, Yanga na Azam. 

Kuelekea msimu mpya, Simba, iliyotoka ndani ya tatu bora imejiimarisha baada ya kupata viongozi wapya- Yanga na Azam bado wapo vizuri. Mbeya City iliyomaliza nafasi ya tatu imejiimarisha pia, timu zilizokuwa nje ya nne bora nazo zimejiimarisha. Zilizopanda nazo kadhalika. Tarajia ligi moja tamu sana.

Karibu Ligi Kuu, kilele cha ladha ya soka ya Tanzania. Zingatia, naitwa Mahmoud Ramadhani Zubeiry, au BIN ZUBEIRY, ndiye nimeandika makala haya. Furahia msimu mpya wa Ligi Kuu.


No comments: