Wednesday, December 10, 2014

HUYU NDIYE MUUZA CHIPS ALIYETUNUKIWA NISHANI YA USHUPAVU NA RAIS KIKWETE

 Rais Jakaya Kikwete akimvisha Nishani ya Ushupavu Kassim Said Kassim ambaye ni muuza Chips katika maeneo ya Buguruni jijini Dar es Salaam, Kassim alitunukiwa Nishani hiyo baada ya kupambana na jambazi aliyevamina na kupora wateja katika eneo la biashara yake na kumpiga chepe na kusababisha kupatikana kwa bastola moja pamoja na risasi tano.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumanne, Desemba 9, 2014 ametunuku Nishani ya Ushupavu kwa mfanyabiashara ya kukaanga na kuuza viazi (chips) wa Dare s Salaam , Bwana Kassim Saidi Kassim, kwa kitendo chake cha kuokoa wananchi dhidi ya jambazi. 

Bwana Kassim Saidi Kassim alikuwa mmoja wa watunukiwa 28 wa nishani mbali mbali ambazo Rais Kikwete alitunuku ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Miaka 53 ya Uhuru.
Katika sherehe ya kutunuku nishani iliyofanyika kwenye Bustani za Ikulu


Rais Kikwete alieleza kuwa amemtunuku Bwana Kassim Nishani hiyo kwa sababu ya kitendo cha ushupavu alichokionyesha cha kujitoa mhanga kukabiliana na jambazi mwenye silaha ambaye angeleta madhara makubwa. 

Katika maelezo yaliyosomwa kabla ya Rais Kikwete kumtunuku Nishani hiyo, ilielezwa kuwa mnamo Julai 7, mwaka jana, 2013, majira ya saa 3:15 usiku, Bwana Kassim akiwa katika eneo lake la biashara, alitokea jambazi akiwa na silaha aina ya bastola na kuanza kuwashambulia wateja kwa kuwapiga makofi na kuwapora mali zao na fedha zao.

 Iliendeleza kuelezwa: “Kwa ushupavu mkubwa ulichukua chepe na kumpiga jambazi huyo mara mbili kichwani, kipigo kilichosababisha aanguke na kupoteza fahamu. Kitendo hicho kilifanikisha kukamatwa kwa bastola aina ya Glock ambayo nambari zake zilikuwa zimefutwa ikiwa na risasi tano ndani yake na hivyo kuepusha madhara ambayo yangeweza kusababishwa na matumizi mabaya ya silaha hiyo.” 

Bwana Kassim anakuwa muuza chips wa kwanza katika historia ya Tanzania kutunukiwa Nishani ya Ushapavu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Bwana Kassim mwenye umri wa miaka 28 alizaliwa katika Kijiji cha Namwinyu, Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma mwaka 1986. 

Alisoma na kumaliza elimu yake ya msingi mwaka 2002 katika Shule ya Msingi ya Ilala, iliyoko Wilaya ya Ilala, Dar Es Salaam. 

Baada ya kumaliza elimu ya msingi, alianza kujishughulisha na biashara ya kukaaga na kuuza viazi (chips) katika eneo la Buguruni Malapa. 

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
10 Desemba,2014

No comments: