Thursday, December 4, 2014

KAMISHNA KOVA AWATAKA ASKARI WALIOMALIZA MAFUNZO YA UONGOZI MDOGO WA JESHI LA POLISI KUTUMIA UJUZI NA MAARIFA WALIYOYAPATA KUONDOA KERO NA KUDUMISHA AMANI KATIKA MITAA YOTE YA JIJI LA DAR


 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam,Kamishna Suleiman Kova akifurahi jambo wakati akizungumza na Askari Polisi waliomaliza Mafunzo ya uongozi mdogo wa Jeshi la Polisi katika vyuo vya Polisi vya Moshi na Zanzibar,wakati alipowapokea leo Desemba 4,2014 katika Kituo cha Kati cha Polisi,Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Askari Polisi waliomaliza Mafunzo ya uongozi mdogo wa Jeshi la Polisi katika vyuo vya Polisi vya Moshi na Zanzibar wakimsikiliza Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam,Kamishna Suleiman Kova,wakati akiwaasa maswala mbali mbali yahusuyo Jeshi hilo.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam amewapokea askari waliomaliza mafunzo ya uongozi mdogo wa Jeshi la Polisi katika vyuo vya Polisi vya Moshi na Zanzibar ambao ni utaratibu wa kawaida na kuwaasa mambo yafuatayo:
• Amewataka kutumia ujuzi na maarifa walivyopata katika mafunzo yao ili kuondoa kero za uhalifu katika jiji la Dar es Salaam. “Matukio ambayo ni kero katika jiji la Dar es Salaam ni pamoja na matumizi ya Dawa za kulevya, ujambazi wa kutumia silaha, na kero nyingine, madanguro, grocery katikati ya barabara, na muziki unaopigwa kiholela katika makazi ya watu”. Alisema Kamishna Kova.

• Aliwataka washirikiane na askari wenzao katika oparesheni inayoendelea jijini Dar es Salaam kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba ili kuthibiti vitendo vya uhalifu ambavyo kwa kawaida hujitokeza kwa wingi katika kipindi hicho. 

• Aidha, wahitimu hao wametakiwa kusimamia na kudumisha nidhamu katika Jeshi la Polisi ili kuwafanya wananchi wapate huduma nzuri pamoja na kuleta  taswira nzuri ya Jeshi la Polisi.

• Amewaasa askari hao kufuata maadili ya kazi ya Polisi na kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwani wanaweza kupata vyeo vya juu, kuwa mfano na wakawa viongozi bora Jeshini.

Mwisho amewataka kushirikiana na wananchi katika mitaa mbalimbali na kufanya doria ili kila mtaa jijini Dar es Salaam uwe huru dhidi ya uhalifu.


S. H. KOVA,

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,

DAR ES SALAAM.

No comments: