MAAJABU YA COCA,SASA UNAWEZA KUPATA SODA YENYE JINA LAKO


Meneja Mkazi wa Coca-Cola Tanzania Yebeltal Getachew (katikati), Menaja wa mauzo na soko wa Coca-Cola kwanza Nalaka Hettiarachchi(Kulia) na meneja Bidhaa wa Coca-Cola Tanzania Maurice Njowoka(Kushoto) wakionyesha chupa za Coca-Cola zikiwa na majina ya wateja katika uzinduzi wa kampeni ya Share a Coke leo jijini Dar-es-salaam.

Meneja Bidhaa wa Coca-Cola Tanzania Maurice Njowoka akionyesha chupa za Coca-Cola zikiwa na majina ya wateja katika uzinduzi wa kampeni ya Share a Coke leo jijini Dar-es-Salaam.

Meneja Mkazi wa Coca-Cola Tanzania Yebeltal Getachew akizungumza  na waandishi wa habari katika uzinduzi wa kampeni ya Share a Coke leo jijini Dar-es-salaam.Hebu fikiria utajisikiaje inapotokea mtu maarufu akakutambua na kukutaja jina lako katikati ya umati mkubwa wa watu! Ni furaha iliyoje, kwani sasa Kampuni ya Coca-Cola inatoa fursa hiyo kwa wateja wake kupitia kampeni mpya inayojulikana kama ‘Share a Coke’.


Kampeni hiyo inatoa fursa kwa wateja wa Coca-Cola kuweka majina ya marafiki, ndugu au familia zao kwenye sehemu ya nembo ya maarufu ya Coca-Cola. Kampuni ya Coca-Cola imechapisha zaidi ya majina 200 ambayo ni maarufu miongoni mwa vijana wa Kitanzania.

Katika hatua ya uzinduzi wa kampeni hiyo mpya, Kampuni ya Coca-Cola iliweza kuwafurahisha wapenzi wake hususani vijana wenye ushawishi kutoka katika vyombo vya habari na burudani pamoja na mashirika kwa kuwapatia kinywaji murua cha Coke huku kopo la kinywaji hicho likionyesha majina yao ikiwa ni hatua ya kampeni hiyo ya aina yake na ya kipekee.

Katika hafla ya kutangaza uzinduzi wa kampeni hiyo inayosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa Coke, waandishi wa habari, wamiliki wa blog na wenye mitandao ya kijamii, walipata fursa ya kupata kinywaji hicho murua huku makopo ya Coke yakionyesha majina yao, hali inayoashiria kuwa kinywaji hicho ni maalum kwao! Kwa mujibu wa maofisa wa Kampuni ya Coca-Cola, hatua hiyo inalenga kuleta furaha ya pamoja na wapenzi wao kwa miezi minne ijayo.

“Share a Coke inatoa fursa na uzoefu wa pekee kwa wateja wetu na kuwafanya wajisikie raha kwani Coke inakuwa imetengenezwa mahsusi kwa ajili ya mteja mwenyewe ambaye kampuni inamthamini zaidi. Kupitia kampeni hii, tutaendelea kusambaza furaha zaidi kwa wateja wetu majumbani, katika mijumuiko ya kijamii, shuleni, vijijini na migahawa huku tukiendelea kuwaunganisha watu pamoja,” alisema Yebeltal Getachew ambaye ni Meneja Mkazi wa Coca-Cola Tanzania.

Licha ya kuwa kampeni hii ya Share a Coke inawalenga zaidi vijana, inatoa pia fursa kwa wateja wote wa Coca-Cola kuamua na kufurahi na watu muhimu katika maisha yao kwa kunywa kinywaji wakipendacho cha Coke huku kopo likiwa na jina watakalo kulingana na utashi wao. Miongoni mwa majina maarufu 200 yanayotumiwa na vijana kama vile Chris badala ya Christopher au Jerry badala ya Gerald ni kati ya mambo yaliyo katika kampeni hii. Aidha, ipo fursa kwa wateja kuamua mengine zaidi kadri wapendavyo.

Meneja Masoko wa Coca-Cola Tanzania, Maurice Njowoka, anasema kuwa Kampuni hiyo itapanua zaidi kampeni hiyo kupitia mitandao ya kijamii ili kuwawezesha wateja kupata nafasi ya kuchagua majina wanayoyataka wakati wowote huku wakiburudika na kinywaji hicho. Kwa wale wenye shughuli mahsusi kama vile harusi au sherehe za kumbukumbu ya jambo fulani pia wana nafasi nzuri ya kupata kinywaji cha Coca-Cola kikiwa ndani ya makopo yaliyoandikwa majina ya washiriki katika hafla husika.

“Coca-Cola ni kinywaji kinacholeta burudani kwa kila mmoja. Kwa mantiki hiyo, tunahakikisha kuwa Watanzania wanapata fursa ya kuamua juu ya nani wafurahi naye pamoja kupitia kinywaji cha Coke popote pale walipo,” alisema.

Bidhaa za Coke zenye majina maalumu kulingana na utashi wa mteja zinapatikana katika maduka makubwa ya rejareja, maduka ya kawaida au vioski, hoteli na migahawa katika maeneo yote nchi nzima. Aidha, Njowoka alisema kuwa kampeni hiyo itajumuisha pia misemo maarufu inayotumika mitaani kama vile ‘Mshkaji’ na mingine mingi ili kupanua wigo zaidi na kutoa fursa kwa wateja kuwa karibu zaidi na watu wawapendao.

Kampuni ya Coca-Cola itatoa fursa hiyo kwa wateja kwa kuishirikisha mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter au Instagram pamoja na majukwaa mengine yanayotoa fursa za matangazo ya biashara ili kuwawezesha wateja kukata kiu yao kadri wapendavyo. Wateja wataweza si kuagiza tu Coke yenye jina lake, bali pia mteja ataweza kutuma picha, au video za matukio ya kukumbukwa kwenye mitandao ya kijamii akitumia jina la kampeni kupitia: #ShareACokeTZ.

Coca-Cola ikiwa ni Kampuni ya vinywaji baridi inayoongoza duniani, inajulikana sana kwa kuongoza soko la Tanzania kwa kampeni na ubunifu katika masoko. Hivi karibuni imefanikiwa kuzindua kampeni mbalimbali zilizofanikiwa sana. Miongoni mwa kampeni hizo ni pamoja na Sababu Bilioni za Kuiamini, Upande wa Coke wa Maisha, Brrrr na nyinginezo ambazo zilipokewa vizuri na wateja wa Tanzania.

Mwisho…/

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.