Tuesday, January 6, 2015

SHEKH PONDA ANYIMWA DHAMANA,POLISI WATUMIA NGUVU KUWATULIZA WAFUASI WAKE

                                Sheikh Ponda Issa Ponda

Jeshi la Polisi limefanikiwa kudhibiti vurugu zilizotaka kutokea baada ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Sheikh Ponda Issa Ponda kunyimwa dhamana katika kesi inayomkabili.


Tukio hilo limetokea baada ya mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro kupinga maombi ya dhamana kutokana na kuwepo kwa hati iliyotolewa na mkurugenzi wa mashitaka nchini DPP iliyotaka mshtakiwa huyo kutopewa dhamana.
Jeshi la polisi kwa kutumia askari kanzu na FFU waliokuwa na mbwa, silaha za moto pamoja na marungu walilazimika kuimarisha ulinzi mkali katika eneo la mahakama hiyo kwa kile kilichohofiwa kuzuka kwa vurugu baada ya Sheikh Ponda kunyimwa dhamana.
Hali ya vurugu ilionekana kujitokeza baada ya Sheikh Ponda kufikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3: 20 asubuhi kwa kutumia gari dogo aina ya Toyota Carina na hivyo wafuasi hao wa Sheikh Ponda kutaka kuingia ndani ya mahakama hiyo kushuhudia kesi hiyo inavyoendeshwa ambapo askari mmoja alijeruhiwa mkononi kwa kuchanwa na kiwembe.

Askari walilazimika kutumia nguvu kuwazuia na kuwatuliza nje ya uzio wa mahakama huku wafuasi hao wakiendelea kusoma dua na kumuomba Mungu ili kiongozi wao aweze kuachiwa kwa dhamana.
Dhamana moja ya maombi matatu yaliyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi Desemba 22 kupitia wakili Juma Nasoro akishirikiana na wakili Bathoromeo Tarimo na Abubakar Salimu ambao wanamtetea Sheikh Ponda katika kesi inayomkabili mahakamani hapo.
Maombi mengine yaliyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi yalikuwa ni kubadilishwa kwa hati ya mashtaka baada ya Sheikh Ponda kushinda rufaa yake katika mahakama kuu na kupanga tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo iliyoendeshwa kwa zaidi saa mbili, mawakili wa pande zote mbili walionekana kutokubaliana hasa katika suala la kubadilisha hati ya mashtaka, hali iliyosababisha hakimu wa mahakama hiyo Mary Moyo kusitisha mahakama mara mbili kwa dakika 15 ili kutoa nafasi kwa mawakili hao kujadiliana na kutoa maamuzi.

Wakili Kongora alidai kuwa shitaka la kwanza linalomkabili Sheikh Ponda ni la kupinga amri halali iliyotolewa na mahakama ya kisutu Mei 9, 2013 ambayo ilitokana na hukumu iliyomtaka Sheikh Ponda kutohusika na uchochezi na badala yake kuhubiri amani.
Imedai kuwa amri hiyo ilivunjwa na Sheikh Ponda baada ya kuhusika na kutoa maneno ya uvunjifu wa amani na uchochezi kosa ambalo alilifanya katika eneo la kiwanja cha ndege manispaa ya Morogoro ambapo pamoja na shitaka hilo pia alishitakiwa kwa kosa la madai ya kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini nyingine na kushawishi na kutenda kosa.
Wakili Kongora alidai kuwa upande wa mashitaka utaendelea na mashtaka yote matatu na kwamba yote yataweza kuthibitishwa mahakamani hapo kupitia kwa ushahidi na hivyo aliiomba mahakama kuridhia maombi ya kusikilizwa kwa ushahidi huo Januari 26 na 27 mwaka huu.

Kuhusu dhamana hakimu Moyo amesema kuwa mshtakiwa ataendelea kukaa rumande hadi mkurugenzi wa mashtaka DPP atakapotengua maamuzi yake kupitia hati aliyoiwasilisha mahakamani hapo ya zuio la dhamana na kwamba hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutengua hati hiyo ya DPP mpaka kesi itakapomalizika

No comments: