Tuesday, February 10, 2015

HABARI KAMILI KUHUSU MOTO ULIOZUKA LEO JIJINI DAR ES SALAAM


MOTO umezuka mapema leo na kuteketeza majengo matatu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika makutano ya Mtaa wa Libya na Mosque jijini Dar es Salaam.

Moto huo ulioanza majira ya saa tatu asubuhi kwa kuanza kufuka moshi na baadae kuwaka na kuteketeza eneo lote la juu ya majengo hayo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika eneo la tukio Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishina wa Jeshi la Polisi Suleiman Kova amesema vikosi vya uokoaji na Zima Moto vimefanya ushirikiano katika kuzima moto huo baadhi ya maeneo na kuokoa maduka katika majengo hayo.

 ‘’Vikosi vya zima moto vimefanya ushirikiano kwa kuleta magari sita ya kuzima na uzimaji na kufanikisha kuuzima moto ambao ulikuwa mkubwa’’amesema Kova.

Kova amesema kuwa vikosi vya ukoaji vya zima moto vimefanya kazi kwa ushirikiano ambavyo ni  Zima moto za Uwanja wa Ndege,Zima Moto ya Kampuni ya Ulinzi ya Altimate,Night Support ,pamoja  na Kikosi cha Zima moto ya Jiji.

Amesema kuwa  chanzo cha moto bado hakijafahamika mpaka sasa.Amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto huo bado unaendelea .Aidha Kamanda Kova amesema thamani ya vitu vilivyoungua katika majengo hayo bado wanaendelea na uchunguzi lakini hakuna maafa katika moto huo.

Naye Kamishna msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Kanda Maalum ya Dar es salaam,Jeswald Nkongo amewataka wananchi kutoa taarifa mapema pindi waonapo matukio ya moto na sio kudharau kwa kuamini kuwa moto ni mdogo na wanaweza kuudhibiti.
PICHA ZOTE NA OTHMAN MICHUZI NA HAMIS MAKUKA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalim ya Dar es Salaam,Kamishna Suleiman Kova akizungumza na vyombo vya habari.

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Jeswad Nkongo akizungumza na vyombo vya habari juu ya walivyofanikiwa kuudhibiti moto huo

No comments: