Monday, February 23, 2015

HABARI KUBWA,----SOMA ALICHOKISEMA KOVA KUHUSU VIONGOZI WA JKT WALIOTAKA KUANDAMANA

Mwenyekiti wa vijana hao ambaye alikutwa akiwa amepigwa sana baada ya kutekwa hivi majuzi


MWENYEKITI WA UMOJA WA WAHITIMU WA JKT NA KATIBU WAKE WASHIKILIWA NA POLISI KWA MAKOSA YA UCHOCHEZI NA MIKUSANYIKO ISIYO HALALI JIJINI DAR ES SALAAM.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limewakamata vijana wapatao watano wanaojiita viongozi wa “Umoja wa Kikundi cha wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa” kwa makosa ya uchochezi na mikusanyiko isiyo halali jijini Dar Es Salaam. Watu hao wanatabia ya kujikusanya kwenye kundi la vijana wasiopungua 300.

Lengo la mikusanyiko hiyo ni kutaka kuandamana kwenda Ikulu kumwona  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ili awapatie majibu ya tatizo la ajira ya kudumu ambali ndiyo madai yao.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa umoja huo hauna usajili kisheria na hakuna ahadi yeyote ambayo kikundi hicho kimepewa.

Wanaohojiwa mpaka sasa ni pamoja na Mwenyekiti wa kikundi hicho aitwaye GEORGE S/O GALUS MGOBA, Miaka 28, Mkazi wa Mabibo Loyola.

Mwingine ni Katibu wa kikundi hicho aitwaye LINUS S/O EMMANUEL, Miaka 28, Mkazi wa Tabata.
 Aidha, GEORGE S/O GALUS hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa madai kwamba alitekwa nyara huko Mabibo Mwisho tarehe 16/02/2015 hadi alipopatikana tarehe 19/02/2015 majira ya saa nne usiku huko Tumbi Kibaha kando ya barabara. Mtuhumiwa huyo yupo chini ya ulinzi wa Polisi kwa makosa yaliyotajwa hapo juu.
Mnamo tarehe 22/02/2015 majira ya saa 11:45 jioni mtuhumiwa GEORGE S/O GALUS akiwa chini ya ulinzi alijaribu kutoroka kutoka wodini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa lakini Polisi walimbaini na kumkamata kabla hajatokomea. Jalada la utoro chini ya ulinzi halali limefunguliwa na uchunguzi linaendelea.
     
Aidha tukio la mtuhumiwa GEORGE S/O GALUS kudai kutekwa kati ya tarehe 16/02/2015 hadi 19/02/2015 linaendelea kuchunguzwa kwa ushirikiano kati ya Mkoa wa Pwani na Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo na kuwajua wanaosemekana kumteka.

KUJISALIMISHA

Wakati huo huo  Makamu Mwenyekiti wa umoja wa vijana waliohitimu JKT anayejulikana kwa jina la PARALI S/O ARUWERA KIWANGO, Miaka 25, Mkazi wa Temeke Mikoroshini, anatakiwa kujisalimisha haraka katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Polisi Kanda Maalum Dar es salaam au kituo chochote cha Polisi cha karibu na mahali aliko. Mtuhumiwa huyo alitoroka baada ya kugundua katibu wake amekamatwa hivyo anatakiwa ajisalimishe kuhojiwa kwa matukio hayo.

Katika suala hili la wahitimu wa JKT, kuanzia sasa Jeshi la Polisi litachukua hatua kali kudhibiti mkusanyiko au mkutano wa aina yeyote kwani haina uhalali wowote kisheria. Imegundulika kwamba mikusanyiko ya vijana hawa ni uchochezi na siyo halali kisheria hivyo haikubaliki. Yeyote atakayejaribu kushiriki katika mkusanyiko wa aina hiyo awe ni kiongozi au mjumbe atachukuliwa hatua kali haraka sana.
Mpaka sasa baadhi ya wajumbe wafuatao wamekamatwa kwa makosa ya mikusanyiko hiyo ambao ni;

1. EMMANUEL S/O RICHARD, Miaka 28, Mkazi wa Kawe
2. JACOB S/O JOSEPH, Mika 36, Mkazi wa Mabibo
3. RIZIONE S/O NGOWI, Miaka 27, Mkazi  wa Mtoni Mtongani
4. LINUS S/O EMMANUEL, Miaka 28, Mkazi wa Tabata Katibu Mkuu
Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa makundi yeyote ya aina hiyo kuacha kujitokeza na kufanya mikusanyiko au mikutano kwani mikutano ya aina hiyo itachukuliwa ni kunyume cha sheria na hatua zitachukuliwa bila ajizi.

Uchunguzi wa awali wa mashauri hayo utakapokamilika majalada yao yatapelekwa kwa mwanasheria wa serikali kabla ya kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments: