Friday, February 20, 2015

TANZANIA KUIVAA KENYA JUMAMOSI.

http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2015/01/beach-soccer-final.jpg

Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni (Beach Soccer) kesho jumamosi itacheza mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Taifa ya Kenya, mchezo utakaoanza majira ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Escape One Club Msasani jijini Dar es salaam.

Wageni timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni kutoka nchini Kenya wanatarajia kuwasili leo jioni jijini Dar es salaam, tayari kabisa kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano siku ya jumamosi na watafikia katika hoteli ya Saphire iliyopo eneo la Gerezani – Kariakoo.

Katika mchezo wa awali uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mombasa, timu ya Taifa ya Tanzania iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 5 – 3 dhidi ya wenyeji timu ya Taifa ya Kenya na kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele katika hatua inayofuata.



Waamuzi wa mchezo huo watakua ni , Beye Mbokh kutoka Senegal, mwamuzi wa pili ni Signate Youssouph (Senegal), mwamuzi wa tatu, Maolidy Tsaralaza kutoka Madagascar, mtunza muda (time keeper)  atakua Hachim Said Nassur (Madagascar) na kamishina wa mchezo atakua Roch Henriette kutoka Visiwa vya Shelisheli.

Tayari waamuzi wa mchezo huo wameshawasili jijini Dar e salaam tangu jana jioni tayari kwa mchezo huo, na endapo timu ya Taifa ya Tanzania itasonga mbele, itakutana na timu ya Taifa ya Misri kati ya Machi 7, 8 na kurudiana kati ya Machi 13, 14, 2015.

Fainali za Soka la Ufukweni zinatarajiwa kufanayika mapema mwaka huu katika Visiwa vya Shelisheli.


TWIGA STARS KUINGIA KAMBINI JUMAPILI.
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars), Rogasian Kaijage ametangaza kikosi cha wachezaji thelathini (30) kitakachoingia kambini siku ya jumapili kujiandaa na mchezo wa kufuzu Mataifa Afrika dhidi ya Zambia mwezi Machi mwaka huu.

Kaijage ametangaza program yake ya  mazoezi itakayochukua takribani wiki nne (4) ili kuhakikisha wachezaji wanakua tayari kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kati ya Machi 21, 22 mwaka huu, huku akipanga kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuelekea Lusaka Zambia kwenye mchezo wa awali.

Twiga Stars ambayo itakua kambini katika Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF zilizopo Karume,  imeingia moja kwa moja katika hatua ya pili kucheza na Zambia kufuatia kuwa na matokeo mazuri katika msimamo wa viwango vya soka la wanawake barani Afrika.

Wachezaji walioitwa ni, Asha Rashid, Esther Chaburuma, Fatuma Bushiri, Fatuma Hassan, Fatuma Mustapha, Fatuma Omari, Eto Mlenzi, Mwajuma Abdallah, Sofia mwasikili, Zena Khamis, Mwanahamis Omar, Fatuma Khatibu, Fadhira Hamad, Anastazia Anthony, Shelder Boniface.

Wengine ni Thereza Yonna, Happines Hezron, Amina Ally, Donizia Daniel, Fatuma Issa, Vumilia Maarifa, Maimuna Hamisi, Najiati Abbasi, Stumai Abdallah, Ziada Ramadhani, Zuwena Aziz, Irene Joseph (Mfunzo – Zanzibar), Dawa Haji Vuai (JKU – Zanzibar), Belina Julius na Amina Ramadhani.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: