Sunday, February 8, 2015

WAZIRI MEMBE ALIPONGEZA KANISA LA SDA.

1
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Benard Membe akifanya mazungumzo na Rais wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani Askofu Ted Wilson wakati wa siku ya ufungaji wa Kongamano hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku ya tarehe 7 Februari, 2015.
2
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Benard Membe ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwahutubia wananchi pamoja na wageni wengine waalikwa (hawapo pichani) wakati wa siku ya ufungaji wa Kongamano hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku ya tarehe 7 Februari, 2015.
3
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Benard Membe (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Makanisa ya Wasabato (SDA) wakati wa siku ya ufungaji wa Kongamano hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
4
Watoto wakitoa burudani mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa siku ya ufungaji wa Kongamano hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………..

Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dar es Salaam.

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe amelipongeza Kanisa la Wasabato (SDA) kwa kuwa mfano mzuri wa ustahimilivu, uvumilivu wa kidini na imani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Membe ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akifunga rasmi Kongamano la siku 4 (4-7 Februari, 2015) Kimataifa la Utume kwa Kanisa la Sabato  lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambalo lilishirikisha Mataifa zaidi ya 20 Duniani.
Alisema kuwa, katika kipindi chote cha uongozi wake kama Waziri hajawahi kusikia mgogoro wala matatizo yakioongozwa na SDA dhidi ya madhehebu mengine ya dini hapa nchini na hata dhidi ya wananchi.
“Mpo mnafanya kazi zenu, mnachapa shughuli zenu kwa amani na utulivu, hamjachokoza mtu na hiyo ni sifa ya dini mojawapo yenye amani duniani”, alisema Mhe. Membe.
Alisisitiza kwa kuwataka wananchi wa dini zote nchini kuiga mfano wa wana SDA ili Tanzania iendelee kuwa nchi yenye amani na utulivu.
Aidha, alieleza kuwa, Dini na Diplomasia vina husiana pale masuala ya amani, ulinzi na usalama yanapoguswa huku akiwataka wananchi wa dini zote nchini kushiriki katika kutengeneza viongozi bora katika jamii kwa misingi ya uadilifu ambao watasimamia amani na kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa.
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana nalo kwa ajili ya ustawi wa nchi huku akieleza kuwa, Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa dini zote kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya Jamhuriu ya Muungano wa Tanzania.
Naye Rais wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani, Askofu Ted Wilson alisema kuwa anawaombea  Viongozi wa Tanzania waendelee na maono kwa lengo la kuwatumikia wananchi  na kwamba wakimtumaini Mungu atawawezesha kupata maono mapya kwa ajili ya kulitumikia Taifa zima.
Kongamano hilo lilishirikisha Mataifa zaidi ya 20 ambapo Kanisa hilo la Wasabato ni Kanisa linalokua duniani likiwa na Waumini milioni 307 huku Waumini milioni 30 wakiwa Afrika na takriban milioni 5 wakiwa Tanzania.

No comments: