Monday, March 16, 2015

Balozi Juma Mwapachu awa Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Airtel Tanzania

KAMPUNI tanzu ya Bharti Airtel inayoongoza katika utoaji wa huduma za
simu za mkononi ikifanyakazi katika nchi 20 Asia na Afrika, leo
imemteua Balozi Juma Volter Mwapachu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Airtel Tanzania.

Balozi Mwapachu ni Katibu Mkuu aliyepita wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, nafasi aliyoishika kati ya Aprili 2006 na Aprili 2011.
Kabla ya uteuzi huu, Mwapachu alikuwa Balozi Mwakilishi Ufaransa na
UNESCO.

Mwapachu ni mhitimu wa shahada ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSN). Pia ni mhitimu wa Diploma ya Juu ya Sheria ya Kimataifa,
Masuala ya Diplomasia ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Sheria za
Kimataifa na Diplomasia huko New Delhi, India.

Pia ana shahada mbili za heshima katika fasihi na sayansi ya siasa za
UDSM na Chuo Kikuu cha Taifa Rwanda.

Akizungumzia uteuzi huo, Christian de Faria, Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Airtel Africa, alisema: “Ni faraja kwetu Balozi Mwapachu kuiongoza
Bodi yeti ya Wakurugenzi nchini Tanzania. Uzoefu wake mkubwa utaongeza
thamani kubwa kwa Bodi yetu na kutoa miongozo bora ya kimkakati katika
shughuli zetu nchini Tanzania. Tunaamini pia kuwa atadumisha mahusiano
na wadau mbalimbali nchini.”

Kwa upande wake, Balozi Mwapachu alisema: “Ninaipokea kwa heshima
kubwa fursa hii ya kujiunga na Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel, na, kwa
pamoja na wajumbe wenzangu wa Bodi hii ya wakurugenzi wa Airtel,
tutashirikiana  kujenga kampuni thabiti yenye misingi imara ili
kuendelea  kutoa huduma bora ya mawasiliano nchini Tanzania.

“Sekta ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika kukua kwa uchumi wetu
ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wananchi kila mahali. Pia ukuaji wa
teknolojia ya hali ya juu na ubunifu katika masoko ikisaidiwa na mfumo
mzuri wa usimamizi wa sekta hii ni dhahiri kutakuwa na uwezekano kwa
sekta hii ya mawasiliano  kuendelea kutoa mchango mkubwa zaidi katika
maendeleo ya taifa.”

Balozi Mwapachu ana uzoefu mkubwa katika masuala ya kuongoza bodi
mbalimbali kwani amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya
Rasilimali Tanzania (TIB) na Shirika la Reli Tanzania (TRC). Pia
alikuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya East African Breweries
Limited, Kenya.

Kwa sasa yumo katika bodi kadhaa za taaasisi binafsi ndani na nje ya
nchi. Ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM). Uzoefu wake wa kiuongozi katika mashirika na sekta binafsi
Tanzania na eneo la Afrika Mashariki utaleta  tija katika uongozi wake
wa Airtel Tanzania.


No comments: