Monday, March 23, 2015

NDIO MAANA WATU HAWAPENDI SIASA--SOMA MWIGAMBA ALIVYOWAHI KUMKASHFU ZITTO WAKIWA CHADEMA


Siasa na maigizo yake. Samson Mwigamba aliye Katibu Mkuu wa ACT-Tanzania amewahi kuandika makala hii kuhusu Zitto ambaye amejiunga nao, akimkashifu na kumpinga… ilikuwa tarehe 9//12/2009. Jisomee uone.


MHESHIMIWA Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CHADEMA katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, salaam.


Awali ya yote naomba kama nianze kwa kutangaza mgongano wa kimaslahi kama ilivyo kawaida kwa wabunge kufuatana na Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Toleo la Mwaka 2007.


Mgongano wa kimaslahi ni kwamba ninakuandikia waraka huu nikitaka kujadili machache juu ya mwenendo wa mambo ndani ya CHADEMA, mambo ambayo yanakugusa kila wakati nikitaka kujaribu, kwa faida ya wasomaji, kuangalia kulikoni na wakati huohuo nikijua kwamba wewe ni rafiki yangu wa muda mrefu na ambaye tumekuwa pamoja tukikubaliana kwa mambo karibu yote, wakati wote.
Mheshimiwa unajua urafiki wetu ni wa muda mrefu na kwa kweli nilikupenda kabla wewe hujanifahamu; nikakuhesabu kama rafiki kabla hujanifahamu na kwa bahati nzuri sana uliponifahamu ukakubali kuwa rafiki yangu. Nimekuunga mkono katika matukio, maamuzi na hata mitazamo yako mingi kwa muda mrefu.

Nilikuwa upande wako katika kupiga vita ufisadi na hata uliposimamishwa ubunge wakati wa hoja ya Buzwagi nilikuwa upande wako.


Nilikuwa upande wako ulipotoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga utaratibu wa kuwachagua wabunge wa Afrika Mashariki na hata katika kile ulichokiita ‘bifu’ kati yako na Spika wa Bunge, lililotokana na hatua yako ya kutoka nje ya ukumbi wa bunge na maneno uliyoyatoa nje ya ukumbi huo kuhusu uwezo wa spika kusimamia kanuni za Bunge.


Nilikuwa pia upande wako uliposimama kumtetea Spika kuhusu hoja iliyotolewa na mwandishi mmoja akipinga uwepo wa Kamati ya Bunge ya Kutunga Sheria katika kanuni mpya za Bunge.


Nilikuwa upande wako pale ulipounga mkono maelezo ya kitaalam ya TANESCO kununua mitambo ya Dowans na hili unalifahamu zaidi maana tulikuwa tukiwasiliana sana na huenda mimi na Absalom Kibanda ni miongoni mwa waandishi wachache sana tuliodiriki kusema waziwazi kupitia kalamu zetu kwamba tunaunga mkono msimamo wako wa kununua mitambo ya Dowans.


Utakumbuka pia siku moja tulipishana mtazamo tulipokuwa tukichangia kwenye mtandao mmoja wa intaneti hoja ya utafiti wa taasisi moja iliyoonyesha kwamba bado Kikwete na CCM ni maarufu kuliko vyama vya upinzani kwa mbali sana.


Unakumbuka kwamba mimi nilitofautiana na wewe kwa hoja za kitaalam zinazohusu utafiti. Lakini baada ya kutoa hoja zako na mimi nikatoa hoja zangu na wewe ukazijibu nilikubaliana na wewe na hatimaye nikawa upande wako.


Lakini katika siku za karibuni nimejikuta nikiwa katika mfululizo wa matukio, mitazamo na maamuzi ya mimi kutokubaliana na wewe. Utakumbuka nilianza kutokubaliana na wewe kuhusu uamuzi wako wa kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa taifa wa CHADEMA.


Nilikutumia barua pepe ndefu sana nikipinga uamuzi huo na kukuomba kwamba ujitoe kwa hoja nyingi ambazo najua unazikumbuka vema.
Kwa bahati mbaya hukujibu ile barua pepe, lakini sikukata tamaa, nikaambiwa nipitie kwa msaidizi wako David Kafulila. Nikafanya hivyo na Kafulila akanihakikishia kwamba kila tunachoongea anakufikishia na kwamba unampa majibu ya kunipatia.



Lakini mheshimiwa unakumbuka kwamba mwishoni kabisa majibu yako yalikuwa ni kwamba hoja zangu zote ulikuwa unazikubali lakini ulishazizingatia kabla hujaamua kujitosa kwenye kugombea uenyekiti na hivyo usingejitoa. Nashukuru kwamba baadaye uliamua kujitoa japo ulikuwa umechelewa.


Mheshimiwa Zitto, nilitofautiana na wewe pia kwa kauli zako ulizokuwa unazitumia kutaka kuwa mwenyekiti wa CHADEMA kabla ya kujiondoa.


Katika moja ya taarifa za habari ulinukuliwa ukisema unatofautiana na Mbowe kwa sababu wewe ni mjamaa wakati yeye ni bepari. Nikawaza na kukumbuka kwamba Agosti 13, 2006 wakati chama chenu kinazinduliwa upya ulikuwepo na ninaamini ulishiriki kikamilifu katika kufanya utafiti, kuchambua na hatimaye kuja na katiba mpya iliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu siku hiyo na kupitishwa kuwa katiba mpya ya chama hicho.


Na kwamba maneno haya yanayosomeka kwenye utangulizi wa katiba hiyo mpya ya CHADEMA yakiwa
yametamkwa kwa kunyanyua mikono na wajumbe wa mkutano huo mkuu, basi yalikuwa ni yako pia: “Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu uliofanyika Agosti 13, 2006, mjini Dar es Salaam, tumeamua kuifanyia mabadiliko Katiba ya 2004 ya Chama chetu cha siasa kitanachoitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kuipa sura inayoendana na mtazamo na msukumo mpya wa falsafa yetu ya Nguvu na Mamlaka ya Umma na Dira na Dhamira ya chama kuanzia 2006 na kuendelea.



“Kuanzia sasa CHADEMA, kitaendeshwa kwa mujibu wa katiba hii sambamba na kanuni, taratibu na maadili ya Chama vitavyotungwa kwa mujibu wa Katiba ili kuimarisha kutetea, kudumisha, na kuendeleza Demokrasia ya kweli na hatimaye kuweza
kuleta maendeleo ya kweli ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa jamii nzima ya taifa la Tanzania.”



Kama na wewe ni miongoni mwa wana CHADEMA waliotamka maneno hayo siku hiyo kwamba: “Kuanzia sasa CHADEMA kitaendeshwa kwa mujibu wa katiba hii sambamba na kanuni, taratibu na maadili ya Chama vitakavyotungwa kwa mujibu wa Katiba hii” nilitegemea uwe umeisoma katiba yenyewe na kuona kwamba ibara ya 3 ya katiba hiyo, ibara ndogo ya 3.B. kifungu cha 3.1.1 kinasema “CHADEMA ni chama cha itikadi ya Mrengo wa kati (center party)”.


Hata kwa elimu ndogo tu maelezo haya yanatosha kuonyesha kwamba chama hiki kinaongozwa kwa itikadi iliyoandikwa ndani ya katiba ambayo ni Mrengo wa Kati na wala si itikadi binafsi ya Mbowe ya ubepari ama ya Zitto.
Kwa imani niliyokuwa nayo kwako na nikizingatia elimu kubwa uliyokuwa nayo, nafsi yangu ikanituma kufikiria kwamba labda ‘wamekunukuu vibaya’. Nilihudhuria mkutano wenu na waandishi wa habari uliokusudia kuzika tofauti zenu na Mbowe na kusonga mbele kama chama.

Pale ulipoulizwa swali na mwandishi mmoja kwamba utawezaje kufanya kazi na Mbowe wakati wewe ni mjamaa na yeye ni bepari; ukajibu kwa namna ambayo haikukata kiu yangu ndipo nikaamini kwamba kumbe hukunukuliwa vibaya bali ni kweli ulisema maneno hayo.


Nilipingana na wewe pia pale ulipoamua kupinga uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA).
Unakumbuka kwamba nilialikwa katika uchaguzi huo miongoni mwa wageni wachache wanafunzi, wanahabari, wanaharakati na watu wa kada mbalimbali walioalikwa kushuhudia uchaguzi ule.


Wakati wa uchaguzi wenyewe utakumbuka mimi na wewe tulikaa meza moja na tulitenganishwa na mtu mmoja tu (Mkurugenzi wa Uenezi Taifa wa CHADEMA, Erasto Tumbo).


Nilitegemea mambo yasiyoendana na sera na kauli mbiu za chama chenu ambazo zinatangazwa hata katika jina la chama (DEMOKRASIA na MAENDELEO) ambayo yalifanyika pale ukumbini uliyaona.
Najua jioni wakati wa kutangaza matokeo hukuwepo lakini nategemea ulipata taarifa za kauli za vijana mbalimbali walizotoa pale wakitaja waziwazi majina ya watu walioharibu uchaguzi ule.


Sikutarajia kama Naibu Katibu Mkuu wa chama upinge hatua ile iliyochukuliwa na msimamizi wa uchaguzi pamoja na kikao kingine chochote cha juu ya msimamizi wa uchaguzi eti kwa sababu tu rafiki yako Kafulila alikuwa anaongoza.


Hilo lilinipa taabu kubwa na naomba uniwie radhi rafiki
yangu lakini nasema ukweli wa nafsi yangu kwamba nilifikia kujiuliza mara mbilimbili kama ungechaguliwa wewe kuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa, hali ingekuwaje?


Na mwisho nilipingana na wewe pale ulipopinga kwenye vyombo vya habari kuvuliwa wadhifa kwa David Kafulila. Kwanza ulionekana umeweka ubaguzi kwa sababu katika maneno yote uliyonukuliwa ulisisitiza juu ya Kafulila peke yake na hukumgusia kabisa Danda Juju wakati wote walivuliwa kwa sababu
zinazofanana.


Lakini kwa sababu Kafulila ni rafiki yako sana, umemwandaa kuwa mbunge na unamuunga mkono katika harakati zake, na ni mbunge mtarajiwa kwa kuwa anakubalika sana jimboni basi ukamtetea na kumsahau ‘mhanga’ mwenzake. Hilo tu linafanya tutofautiane na zaidi sana tunatofautiana kwa kupinga maamuzi ya Katibu Mkuu wako nje ya vikao, maamuzi aliyoyachukua kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.


Najua yote haya umeamua kuwa kimya hujayatolea
kauli yako ikiwa ni pamoja na yale ya kumfadhili Kafulila kwenda Kigoma kuichafua vizuri CHADEMA. Lakini kama ni kweli, napingana na wewe na kama unaendelea kukaa kimya nitaamini kwamba ni kweli.


Sasa limeibuka la kusema kwamba unatembea na barua ya kujiuzulu nyadhifa zako zote ndani ya CHADEMA ikiwa ni pamoja na ubunge. Bado pia sijapata kauli yako, narudia kusema kwa kuendelea kunyamaza unanifanya niamini kuwa ni kweli.


Na kama ni kweli, nakuhurumia sana Zitto Kabwe. Sasa naona kile nilichokuambia wakati nikikushauri ujitoe kugombea uenyekiti kinatimia. Nilikuambia ujitoe haraka tena kimyakimya kwa kumweleza tu Katibu Mkuu aweke fomu yako pembeni lakini hukutaka kunisikia.


Lakini utakumbuka moja ya sentesi zangu ilikuonya kwamba ukingang’ania kugombea iwe umeshinda
uenyekiti ama umeshindwa utapata shida kubwa. Nilikueleza kwamba hutaaminika tena na Watanzania na kila kitu utakachofanya utaonekana kama ulikuwa ni mamluki ndani ya chama.


Ni kwa bahati kwamba umetokea kuwa na viongozi wenye busara sana kina Freeman Mbowe na kina Dk. Wilbrod Slaa wakisaidiwa na hekima na kamati ya wazee.
Hawa wakaamua kukurejesha kwenye unaibu katibu mkuu. Nilishuhudia siku ile wajumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA walivyoshangilia uteuzi wako na wa Dk.


Slaa na Hamad Yusuph kama wakuu wa Sekretarieti ya chama.
Nilidhani sasa ungetulia na kufanya kazi ya kujenga chama chenu na kusonga mbele lakini haikuwa hivyo.

Baada ya kushauriana sana wakati ule ulipotaka kugombea uenyekiti niliamua kutafuta habari za kiuchunguzi ndani ya CHADEMA. Nimeongea na viongozi mbalimbali na maofisa wa CHADEMA makao makuu, nimeongea sana na David Kafulila na hata niliwahi kumsikiliza mama yako mzazi akiongea na watu ambao sikuwafahamu.


Nimegundua kitu kimoja tu: kwamba kama mambo haya huyafanyi kwa makusudi na kwa malengo maalumu, basi watu uliowaamini sana ndani ya CHADEMA hata kama walikuwa na nyadhifa ndogo, walikubali kutumiwa ili wakutumie wewe kuimaliza CHADEMA na wewe ukaingia mkenge.


Ukakubali kugombanishwa na viongozi wenzako wa ngazi za juu hasa Mwenyekiti Freeman Mbowe ili malengo ya watu hao yatimie. Sasa nakuonea huruma.


Nakuonea huruma kwa sababu kama ni malengo ya hao watu kukutumia kukimaliza chama hawatafanikiwa na badala yake watakumaliza wewe bure na utakuja
kushtuka ukiwa umekwisha kisiasa.


Kama ni malengo yako kwa utashi wako umeamua kutumika kukimaliza chama, nakuhurumia kwa sababu utajimaliza wewe na CHADEMA itaendelea kuimarika bila wewe wala Kafulila.


Ukitaka kujua ninachokisema, tuulize sisi waandishi tunaopata mawazo ya Watanzania moja kwa moja. Kwa
kuanzia muulize tu Edward Kinabo kwamba Jumatano iliyopita alipoandika makala ya “Simwelewi Zitto Kabwe” aliungwa mkono na wasomaji wangapi na walikuwa na mawazo gani juu yako. Hapo ndipo utakapoelewa kile ninachokisema.


Namalizia kwa ujumbe wa msomaji wangu mmoja tu kati ya wengi. Huyu aliniambia anaitwa Meshack na yuko Korogwe. Aliniambia, “Sisi tulishajua
kwamba Zitto anaondoka CHADEMA na kwamba anachosubiri tu ni pensheni yake ya ubunge ambayo huwa inatolewa baada ya Bunge kuvunjwa.


Naomba Mwigamba kwa sababu unaweza kuongea na viongozi wakuu wa CHADEMA, waambie kwamba
wasije wakafanya kosa la kumvua Zitto uongozi wala kumvua uanachama.

Sisi hatutaki apate kisingizio cha kuondoka CHADEMA. Waambie wamuache tu mpaka atakapoondoka mwenyewe ili Watanzania wazidi kumfahamu,” mwisho wa kunukuu.


Tafakari mwenyewe ulikofika, uamue cha kufanya. Kumbuka uamuzi wa mwisho ni wako wengine tunakueleza tu maana tumejiapiza kuzungumza ukweli hata katikati ya ugomvi.

Kama utaamua kuondoka CHADEMA ama kujivua tu nyadhifa zako. katika yote nakutakia kila heri!



No comments: