Saturday, April 18, 2015

KUNA KITU KINAENDELEA KATI YA ZITTO NA DK MENGI,NIMEKUWEKEA UDAKU WOTE HAPA


HAPA NI JINSI MENGI ALIPOONYESHA 
WASIWASI WAKE JUU YA MAISHA YAKE

Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi amesema anahofia usalama  wa maisha yake, kufuatia habari iliyoandikwa katika gazeti moja la kila wiki  kwamba,  Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye jambo ambalo limempa hofu kubwa.

         Kadhalika, amelalamikia  Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari Maelezo kwa kukaa kimya na kuacha kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma hizo, huku taarifa hizo zikiendelea kusambazwa.

         Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mengi alisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuwa yeye ni kinara wa kuhujumu serikali ya Rais Kikwete siyo za kweli.

         Dk.Mengi alisema amesoma kwa masikitiko makubwa habari iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na gazeti la Taifa Imara, yenye kichwa cha habari 'Zitto amchongea Mengi kwa JK' ambapo pamoja na mambo mengine inasema kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete kwamba ndiye kinara wa kuhujumu serikali yake.

          Alisema habari hiyo ambayo chanzo chake kimeelezwa kwamba ni Ikulu, iliendelea kueleza kuwa Zitto alikutana na Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow ambayo Zitto alikuwa ni mwenyekiti wake.

       "Habari hiyo inasema kwamba katika mazungumzo yake na Rais Kikwete Zitto amenukuliwa akimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara ni Mengi," alisema Dk. Mengi.

      Dk. Mengi alisema habari hiyo ambayo nakala yake ameiambatanisha kwenye taarifa yake, inasema yeye Zitto , binafsi amekuwa akishawishiwa na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.

     Hata hivyo, Dk. Mengi alisema katika habari hiyo Zitto alikwenda mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa Rais Kikwete akimaliza muda wake wa Urais atamshughulikia kwa nguvu zake zote.

     Alisema habari hiyo imeeleza kwamba baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa taarifa hizo.

    Mengi alisema tuhuma zilizotolewa kuhusu nia yake ya kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko la kwamba Rais Kikwete aliapa kuwa atapambana na yeye zimempa hofu kuhusu mustakabali wa maisha yake.

     Alisema kuwa hofu yake kubwa inasababishwa na Ikulu na Idara ya habari Maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote.

    "Najua umakini wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya habari Maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu Rais, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,"alisema Dk. Mengi.

    Aliongezea kusema kuwa," hofu yangu inazidi kuwa kubwa kwa sababu Rais ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama. Kauli yake kama ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba atapambana na mimi inawezekana kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola kuniangamiza," alisema.

         Alitolea mfano mwaka 1170, Askofu Mkuu wa Canterbury nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia mfalme akisema "hakuna anayeweza kuniondolea huyo mkorofi?". Walinzi wake wakadhani mfalme ameagiza wamuue Askofu huyo na wakamuua, alisema.


MAJIBU YA ZITTO KABWE JUU YA TUHUMA HIZO

Katika gazeti la Taifa Imara la tarehe 23 Machi 2015 kulikuwa na habari yenye kichwa cha maneno ' Zitto amchongea Mengi kwa JK?' Habari hiyo ilibeba maudhui ya 'post' iliyoandikwa katika mtandao wa Mwanahalisi online. 
Habari hiyo inaonyesha kuwa Mimi nilikutana na Rais kwa msaada wa watu mbalimbali na katika kikao hicho inadaiwa nilisema kuwa Mengi ndiye aliyechochea wabunge kuishughikia Serikali ya Rais Kikwete ili ianguke. 

Ni vema ifahamike kuwa gazeti la Taifa Imara linamilikiwa na Bwana James Rugemalira wa kashfa ya Escrow na kuendeshwa na Bwana Prince Bagenda aliye organise press conference ya mmoja wa mawaziri waliofukuzwa kazi kwa kashfa hiyo. Vile vile chanzo cha habari hiyo ni mtandao wa mwanahalisi online ambao unaendeshwa mmiliki wa Mawio gazeti ambalo kila wiki lina habari za kutunga dhidi yangu na chama cha ACT Wazalendo. 

Habari hiyo ni ya kutunga yenye fitna zenye lengo la kuchonganisha watu. Naomba kufafanua ifuatavyo
1 Taarifa Maalumu ya Kamati ya PAC kuhusu ufisadi wa tshs 306 bilioni za Escrow hauhusiki na Bwana Reginald Mengi kwa namna yeyote ile. Mengi sio mbunge, sio mjumbe wa PAC na hakushawishi PAC kwa namna yeyote ile. Wezi wa Escrow wasitapetape kutafuta mchawi wakati mchawi ni wizi wao wenyewe.

 Porojo za kwamba Mengi alihonga wabunge ili kuishughulikia Serikali zinabaki porojo tu. Ila kama kuna mtu ana chembe ya ushahidi wa jambo hilo apeleke kwenye vyombo vya dola kwa hatua kuliko kurudia rudia porojo hizo kwenye vyombo vya habari. 

2 Sihitaji kutumia watu ili kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwani ninaweza kukutana naye kwa taratibu za kawaida kabisa za kiserikali. Hadithi ya kwamba nimeomba watu wanikutanishe na Rais inaonyesha namna mwandishi alivyoshindwa kutunga uongo wake. Katika kukutana kwangu na Rais kikazi sijawahi hata mara moja kuzungumzia watu. 

Hivyo kusema nilikwenda Ikulu kumzungumzia Bwana Mengi ni kunidharau na kuidhalilisha Taasisi ya Urais. 
3 Nimemwelekeza mwanasheria wangu achukue hatua za kisheria dhidi ya Gazeti la Taifa Imara na vilevile Gazeti la Mawio kwa mfululizo wa habari za kutunga uongo dhidi yangu kila kukicha. Nimeagiza tupeleke mashtaka kwenda Baraza la Habari Tanzania ili magazeti hayo yathibitishe habari zao. 
Zitto Kabwe
Kiongozi wa ACT Wazalendo

No comments: