Friday, July 17, 2015

BASATA WAMLILIA MAREHEMU BANZA STONE


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Msanii wa muziki wa dansi Ramadhan Ally Masanja (Banza Stone) kilichotokea nyumbani kwao Sinza jijini Dar es Salaam leo mchana siku ya Ijumaa ya tarehe 17/07/2015 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Banza Stone ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza muziki wa dansi nchini hasa katika kubuni miondoko mbalimbali ambayo ilikuja kupata umaarufu mkubwa. Moja ya mwondoko uliopata umaarufu mkubwa ni ule wa “Achimenengule” akiwa na Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT).
Mchango wake katika muziki wa dansi hasa katika kubuni na kutunga nyimbo zenye ubora, ujumbe na maadili kwa jamii hautasahaulika kamwe. Ni mwanamuziki aliyeacha misingi katika sekta ya muziki na alijitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki wa dansi mahali ulipo leo.
Itakumbukwa kwamba mnamo Julai 3, 2015 BASATA na Asha Baraka, Mkurugenzi wa African Stars Entertainment (ASET) walichukua juhudi za makusudi kwenda nyumbani kwa msanii huyu kufanya mashauriano na familia yake ikiongozwa na kaka yake Khamis Ally Masanja na hatimaye kwa pamoja kumrejesha tena hospitalini kwa ajili ya matibabu yake.
Hata hivyo pamoja na juhudi hizo za kupigania uhai wake Mungu kampenda zaidi Msanii mwenzetu Banza Stone. Upendo wetu kwake umezidiwa na ule wa mwenyezi Mungu ambaye kimsingi wote tutarejea kwake.
Baraza, wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu Banza Stone hasa katika kupenda kujitolea muda mwingi katika kukuza muziki wa dansi na sekta ya muziki kwa ujumla.
Baraza linatoa pole kwa ndugu wa marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na wadau wote wa Sanaa katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI

No comments: