Wednesday, September 23, 2015

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM DAR ES SALAAM LIMEIMARISHA ULINZI WAKATI WA SIKUKUU YA IDD EL-HAJI



Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam ili kuwawezesha wananchi kusherehekea Sikukuu Kuu ya IDD EL-HAJI itakayosherehekewa leo 25/09/2014 kwa amani na utulivu.  
Katika kuhakikisha haya yanafanyika kwa weledi mkubwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum limejipanga kutekeleza yafuatayo:

·        Kutakuwa na ulinzi wa kutosha kwenye nyumba zote za ibada hususani katika misikiti na maeneo mengine yenye mikusanyiko inayohisiana na siku kuu hiyo.

·        Kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Kikosi cha Zimamoto na uokoaji, Kampuni binafsi za ulinzi, Vikosi vya uokoaji wakati wa majanga, na vikundi vya Ulinzi Shirikishi ili kuhakikisha kuna udhibiti wa matukio ya uhalifu au fujo zinazoweza kujitokeza.

·        Limepanga kutumia kikosi maalum cha intelijensia ili kukusanya taarifa zote muhimu ambazo zitasaidia kuzuia matukio au mipango ya kufanya matukio ya uvunjifu wa amani.

·        Tumejipanga kutumia Kikosi cha FFU kikijumuisha askari na magari ya washawasha, Askari wa Mbwa na Farasi. Kikosi cha Polisi Wanamaji nacho kitakuwepo. Pia askari wa kawaida (GD), askari wa Usalama Barabarani, n.k watakuwepo kila mahali. Wote hawa wamepewa maagizo maalum ya kuchukua hatua kabla matukio ya uhalifu hayajajitokeza na sio kungoja tukio lifanyike. Kwa mantiki hiyo, dalili zozote za uvunjifu wa amani litashughulikiwa bila kuchelewa.

·        Zitakuwepo doria za Miguu na doria za pikipiki  katika barabara zote muhimu.

·        Wananchi wanashauriwa kusherehekiea siku ya IDD EL-HAJI katika ngazi ya familia au kukusanyika katika mitaa wakisherehekea kwa amani na utulivu.

·        Aidha kutokana na sababu za kiusalama na matishio mbalimbali katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, Jeshi la Polisi limepiga marufuku disko toto katika kumbi mbalimbali kutokana na sifa za kumbi hizo kutokidhi viwango vya kiusalama.

·        Wananchi wanapoona dalili zozote au maandalizi ya uvunjifu wa amani watoe taarifa mapema iwezekanavyo katika vituo vya Polisi vya karibu ili hatua zichukuliwe kwa haraka.

·        Aidha, madereva wanatakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, kutoendesha vyombo hivyo wakiwa wamelewa, magari au pikipiki zenye sauti kali/zenye kuleta mshtuko nazo ni marufuku.

·        Aidha, Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine Police) kitafanya doria kwenye fukwe za Bahari na maeneo yote ya Bahari jijini Dar es Salaam.

·        Polisi watatoa ulinzi katika fukwe za bahari, kwa kuweka vituo vya Polisi vya muda vinavyohamishika (Mobile Police Station) ili kutoa msaada wa haraka pindi unapohitajika. Pia askari wa kutosha watakuwepo kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa amani.

“TII SHERIA BILA SHURUTI”
NAWATAKIA NYOTE HERI YA IDD EL-HAJI - 2015

No comments: