Thursday, October 22, 2015

Hofu ya kukatwa kwa Mawasilano ya simu na mtandao Jumapili yatanda-CHADEMA waibuka na onyo kali

Naibu katibu mkuu wa chama cha Democrasia na maendeleo CHADEMA Bwana SALUM MWALIMU akizungumza na wanahabari mapema leo Jijini Dar es salaam
Chama cha Democrasia na maendeleo CHADEMA pamoja na umoja wa katiba ya wananchi UKAWA wamesema kuwa upo mpango unaoandaliwa na chama cha mapinduzi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa wanakata mawasiliano hasa ya mtandao kwa siku ya upigaji kura Tanzania,mpango ambao wamesema kuwa unasukwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa watanzania wanakuwa hawana mawasiliano ya haraka kupenana habari za matokeo na uchaguzi kwa ujumla siku hiyo.

Kauli ya kuhofia swala hilo imetolewa leo mchana jijini Dar es salaam na kaimu katibu mkuu wa chama cha CHADEMA Bwana SALUM MWALIMU ambapo amesema kuwa upo mpango wa kukata mawasiliano ya data na internent kwa muda wa siku hiyo ambao amesema kuwa vikao vya kuamua swala hilo vinaendelea huku akisema kuwa mpango huo unaweza kuvuruga uchaguzi wa Tanzania.

Amesema kuwa mpango huo ni mwendelezo wa vitisho na vihoja mbalimbali ambavyo vinafanywa na watawala kuhakikisha kuwa wanashinda uchaguzi wa mwaka huu kwa njia yoyote ambapo amewataka watanzania kuwa makini na kutotetereka kwa lolote kwani wako makini kwa kila jambo linaloendelea katika uchaguzi hususani kipindi hiki cha kampeni za lala salama.

Salum Mwalimu ambaye pia ni mgombea ubunge wa jimbo la kikwajuni huko Zanzibar ameitaka mitandao ya simu nchini kutokukubali kuingia katika siasa kwa njia hiyo kwani watakuwa wamechangia kuvuruga uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine Naibu katibu mkuu huyo amesema kuwa chama chake pia kimenasa mipango mipya ya watawala ambayo tayari vikao vimefanyika ya kuhakikisha kuwa vijana wa boda boda katika maeneo mengi nchini wanakamatwa na kuwekwa ndani kwa muda hadi uchaguzi upite ili kupunguza kura zao swala ambalo amesema kuwa lilipangwa kuanza leo.

Amesema kuwa swala kama hilo ni kukiuka haki za watanzania wanaotaka kufanya mabadiliko katika uchaguzi wa mwaka huu jambo ambalo linaweza kuwasababishia matatizo makubwa kwa  watawala mara baada ya uchaguzi mkuu.

Ikumbukwe kauli ya kukamatwa kwa boda boda ilitolewa pia jana na mgombea urais wa UKAWA ndugu EDWARD LOWASA akiwa katika kampeni huko tanga ambapo alisema kuwa wapo vijana kadhaa wa boda boda ambao wamewekwa ndani bila makosa maalum huku akiwataka askari na vyombo vya usalama kuacha kutumika kwa stail hiyo kwani kuna maisha baada ya uchaguzi na wanaweza kujikuta matatizoni.


No comments: