Saturday, October 24, 2015

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM LAWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU USALAMA WAO SIKU YA UCHAGUZI 25/10/2015



       Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawataka wananchi wote waliojiandikisha kushiriki kikamilifu kupiga kura ili kutekeleza haki yao ya msingi kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowapenda. Hakuna sababu ya kuwa na hofu siku hiyo kwa vile Jeshi la Polisi limejiandaa vya kutosha kuhakikisha kwamba kuna ulinzi, usalama na utulivu katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na vituo vyote vya kupigia kura.

Tumewasiliana na uongozi wa juu wa Tume ya taifa ya Uchaguzi pamoja na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kwa pamoja tumeweka mikakati ya kutosha ya kudhibiti aina yoyote ya uvunjifu wa amani unaoweza kujikeza.

Kupitia taarifa za kiintelijensia tayari tumebaini mbinu chafu zilizotaka kutekelezwa na watu wachache za kutaka kuvuruga utaratibu mzuri uliowekwa na Tume ya Taifa uchaguzi. Mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kuleta fujo au uvunjifu wa amani wa aina yoyote watachukuliwa hatua kali za kisheria.


Maagizo ya tume pamoja na ya mkuu wa Jeshi la Polisi ya kuzuia mikusanyiko ya aina yoyote baada ya siku ya mwisho ya kampeni tarehe 24/10/2015 yazingatiwe. Kwa ujumla hatutakuwa na uvumilifu wa aina yoyote kwa mtu yeyote atakayejaribu kuwafanya watu waishi kwa hofu kuanzia tarehe 25/10/2015 na badala yake sheria itachukua mkondo wake na wanaohusika watakamatwa bila kufanya ajizi.

Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Ilala, kinondoni na Temeke wamepewa maagizo ya kuhakikisha kwamba wananchi katika maeneo yao wanalindwa kikamilifu ili kundi moja lisiwe tishio kwa kundi lingine na wazingatie ushiriki katika uchaguzi wa makundi maalum ikiwa ni pamoja na  akina mama, walemavu na wazee ambao wana haki sawa na makundi mengine kama vijana n.k. Kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na ulinzi wa kutosha wa Jeshi la Polisi ambapo pia taratibu zote za kupiga kura na kuhesabu kura zitafanyika katika hali ya utulivu.

Kila mtu jijini Dar es Salaam na Tanzania nzima ana wajibu wa kutunza amani na kutoa taarifa za mtu yeyote au kundi lolote ambalo litaenda kinyume na katiba au sheria mbalimbali za nchi ikiwa ni pamoja na sheria zinazolinda haki na demokrasia wakati wa uchaguzi mkuu.

Tunawaomba wananchi wote washirikiane na Jeshi la Polisi bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa ili kila anayestahili kupiga kura apate fursa sawa. Kushinda uchaguzi au kushindwa iwe ni matokeo ya utekelezaji wa demokrasia hivyo tunawaomba watu wa jiji la Dar es Salaam pamoja na watanzania kwa ujumla wawe wavumilivu na aidha kupongezana au kupeana pole katika hali ya amani na utulivu kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.

Napenda kuwatoa wasiwasi wapiga kura wote na watu wengine kwamba wasisite kutekeleza haki yao kwani Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu katika hali ya weledi na uwezo wa hali ya juu kukabiliana na tatizo lolote. Mikoa na Vikosi vyote vya Jeshi la Polisi vimeandaliwa na kuwekwa tayari pamoja na kupata askari wa ziada, vitendea kazi vya kutosha pamoja na matayarisho ya kila aina siku ya tarehe 25/10/2015 ikiwa ni pamoja na Helkopter za Polisi zitakuwa angani ili kuwahakikishia wananchi usalama wao jijini Dar es Salaam.

NB:   Kutokana na maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya jopo la Majaji watatu, baada ya maombi ya Wakili wa vyama vya siasa vya upinzani mahakama hiyo imetoa hukumu na tafsiri dhidi ya maombi ya wakili KIBATALA ambaye alitaka tafsiri ya watu kuzuiwa au kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.

        Katika hukumu hiyo ni kwamba hairuhusiwi na ni marufuku kufanya mikutano eneo la upigaji kura ikiwa ni pamoja na kukaa mita 200. Kutokana na hilo Jeshi la Polisi halitaruhusu mtu au kikundi chochote kukaa au kukusanyika kwa kisingizio cha kulinda kura kwa kuwa mahakama ambayo ni chombo cha kisheria imeshatoa tafsiri sahihi na kwamba kazi ya kulinda kura ni ya mawakala wa vyama na si ya wapiga kura au wanachama wa vyama vya siasa.  Yeyote atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.


S. H. KOVA,

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.

No comments: