Tuesday, October 20, 2015

KIIZA MCHEZAJI BORA WA LIGI YA VODACOM SEPTEMBA


Mshambuliaji wa timu ya Simba, Hamisi Kiiza ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Septemba.
Kwa kuibuka mchezaji bora, Kiiza atazawadiwa sh. milioni moja kutoka kwa mdhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.
Kiiza ambaye ameisadia Simba kufanya vizuri kwenye mwezi huo, ikiwemo kufunga mabao matatu (hat trick) kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar aliwashinda washambuliaji wa timu za Stand United (Elias Maguli) na Yanga (Amisi Tambwe).
Ndani ya mwezi Septemba ambapo zilichezwa raundi tano, Kiiza amefunga jumla ya mabao matano.

Ligi kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku timu 8 zikisaka kupata pointi tatu muhimu.
Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Young Africans watawakaribisha Toto Africans, mchezo utakaonza majira ya saa 10:30 jioni, mjini Shinyanga Stand United watakua wenyeji wa Majimaji katika uwanja wa Kambarage mjini humo.
Tanzania Prisons watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Wagosi wa Kaya, Coastal Union wakiwakaribisha Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakani jijini Tanga.
Alhamis ligi hiyo itanendelea kwa michezo minne pia kucheza katika viwanja mbalimbali, JKT Ruvu wataikaribisha Mtibwa Sugar uwanaj wa Karume jijini Dar es salaam, Mwadui FC watacheza dhidi ya Mgambo Shooting katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.
Jijini Mbeya, Mbeya City watawakaribisha African Sports katika uwanja wa Sokoine, huku Ndanda FC wakiwa wenyeji wa waoka mikate wa bakhresa Azam FC katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi za raundi ya 11 za Ligi Kuu ya Vodacom zilizokuwa zichezwe Novemba 7 na 8 mwaka huu sasa zitafanyika Desemba 12 na 13 kupisha maandalizi ya Taifa Stars ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Taifa Stars inatarajia kuingia kambini mapema mwezi ujao kujiandaa na mechi ya kwanza dhidi ya Algeria ambayo itafanyika Novemba 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana nchini Algeria, Novemba 17 mwaka huu.
Mechi hizo za Vodacom zitakazochezwa Desemba 12 ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga (Tanga), Kagera Sugar na Ndanda (Tabora), Stand United na Mwadui (Shinyanga), Mbeya City na Mtibwa Sugar (Mbeya), Azam na Simba (Dar es Salaam) na Majimaji na Toto Africans (Songea). Mechi za Desemba 13 ni kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons (Dar es Salaam), na Coastal Union na African Sports (Tanga).
Pia mechi tatu za raundi ya sita ambazo hazikuchezwa Oktoba 4 mwaka huu kupisha mechi ya Taifa Stars na Malawi sasa zitafanyika Desemba 16 mwaka huu. Mechi hizo ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam), na African Sports na Yanga (Tanga), mchezo kati ya Ndanda na Simba (Mtwara utapangiwa tarehe ya kuchezwa.

Nayo mechi namba 59 kati ya JKT Ruvu na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Oktoba 21 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam imesogezwa mbele kwa siku moja hadi Oktoba 22 mwaka huu ili kuipa nafasi ya mapumziko JKT Ruvu ambayo jana (Oktoba 18 mwaka huu) ilicheza mechi yake ya raundi saba mkoani Shinyanga
Ligi Daraja la kwanza nchini (SDL) sasa itaanza Novemba 14 badala ya Oktoba 31 ili kutoa fursa kwa bodi ya Ligi kukamilisha maandalizi mengine ikiwemo viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michezo ya ligi hiyo.

No comments: