Tuesday, November 10, 2015

FAMILIA YAVUNJIWA NYUMBA YAKE ARUMERU.

ar1
mkazi wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha,Juma Isangu akiwa na mkewe Janet Tinai pamoja na mtoto wao,Issa Juma(katikati) wakiangalia nyaraka mbalimbali nje ya nyumba yao mara baada ya kufukuzwa na kisha kuvunjiwa nyumba yao juzi wilayani humo na kampuni ya Majembe Auction Mart kwa amri ya mahakama.
ar2
Mkazi wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha,Janet Tinai akilalamika mbele ya waandishi wa habari akiwa na baadhi ya vyombo vyake  mara baada ya kuhamishwa kwa amri ya mahakama na kampuni ya Majembe Auction Mart juzi.
ar3
Mkazi wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha,Juma Isangu akiwa na mkewe,Janet Tinai wakitafakari nje ya nyumba yao mara baada ya kuhamishwa na kisha kuvunjiwa nyumba yao na kampuni ya Majembe Auction Mart kwa amri ya mahakama.
……………………………………………………………………..

Mahmoud Ahmad Arumeru
 
Serikali imeombwa kuingilia kati sakata la familia ya Juma Isangu mkazi wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha kuondolewa na kisha kuvunjiwa nyumba waliyokuwa wakiishi kwa amri ya mahakama kwa madai haki haikutendeka.
 
Familia hiyo iliondolewa juzi majira ya saa 6;30 juzi mchana na kampuni ya udalali wa mahakama ya Majembe Auction Mart Ltd  tawi la Arusha kwa madai kwamba waliagizwa na msimamizi wa mirathi wa nyumba hiyo aitwaye,Janeth Fosbrooke kuwaondoa  kwa kuwa hawastahili kuwepo ndani yake.
 
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo,Isangu akiwa na mkewe,Janet Tinai pamoja na mtoto wao wa kiume,Issa Juma alisema alisema kwamba kwa sasa hawaelewi ni wapi wataishi kwa kuwa kitendo cha kuondolewa katika nyumba hiyo na kisha kutupiwa virago hakikufuata sheria.
 
Alisema kwamba wameondolewa kinyemela ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi bila taarifa ingawa  hapo awali waliwahi kushinda kesi ya mgogoro wa nyumba hiyo nambari 33 ya mwaka 2011 iliyofunguliwa katika mahakama ya ardhi.
 
Akielezea tukio hilo Tinai alisema kwamba mnamo juzi majira ya saa 6;30 mchana watu wapatao sita ambao walijitambulisha kwamba ni madalali  wa mahakama kutoka kampuni ya Majembe Auction Mart walifika katika nyumba wanayoishi wakiambatana na askari wa jeshi la polisi na kuwataka kutoka nje ya nyumba hiyo.
 
Tinai,alisema kwamba wakiwa wanajiuliza ndipo watu hao waliingia ndani na kisha kuanza kutoa baadhi ya mali mbalimbali na kisha kuzipeleka ndani ya lori mojawapo lililokuwa limeegeshwa nje ya nyumba hiyo na kuacha baadhi ya vitu nje ya  eneo la nyumba hiyo.
 
Alisema kwamba na mara walipohoji walijibiwa ya kwamba hawakutakiwa kuendelea kuishi ndani ya nyumba hiyo kwa kuwa kuna  amri kutoka mahakama kuu inayowataka kuondoka mara moja ndani ya nyumba hiyo .
 
Hata hivyo,kwa nyakati tofaiti wanafamilia hao walisema kwamba nyumba hiyo ni halali kwa kuwa walipewa na marehemu Henry Fosbrooke ambaye alikuwa mmiliki halali wa eneo hilo  tangu mwaka  1980 ambaye aliacha wosia waliuwasilisha mbele ya mahakama kuu kanda ya Arusha kama moja ya vielelezo na kisha kukubaliwa.
 
Hatahivyo,Mwenyekiti wa kitongoji cha Duluti,Elias Kaaya akihojiwa na waandishi wa habari katika eneo la tukio alisema kwamba hivi karibuni baadhi ya watu ambao walijitambulisha kwamba ni madalali wa mahakama kutoka  kampuni ya Majembe Auction Mart walifika ofisini kwao na kuwapa taarifa kuwa wataendesha zoezi la kumtoa mpangaji aitwaye,Isangu kwenye kitongoji chake.
 
Huku akionyesha barua ya mnamo Novemba 11 mwaka huu yenye KUMB No,REF.NO.MAM/ARJHF/10/2015  mwenyekiti huyo alidai kwamba watu hao waliomba uwepo wa usimamizi kutoka ofisi yake kumtoa mkazi huyo na kudai waliwasilisha pia taarifa kwake na jeshi la polisi wilayani Arumeru.
 
“Majembe Auction Mart Ltd madalali ya baraza la ardhi na nyumba (Court Blockers) ukiwa msimamizi wa amani kwenye kata yako ya Akheri tunakuomba uwepo katika zoezi la kumhamisha/kumtoa mpangaji ndugu Juma Isangu aliyekuwa amepangishwa na marehemu Henry Albert Fosbrooke ambapo kwa sasa msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa m/s Janeth Fosbrooke ndiye ametuteua kutekeleza zoezi hili la kumtoa mpangaji kwenye nyumba”ilisema sehemu ya barua hiyo
 
Hatahivyo,msimamizi wa mirathi wa nyumba hiyo,Fosbrooke hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini msimamizi wa  kampuni ya Majembe Auction Mart Ltd tawi la Arusha ,Suleiman Mdoe alisema ya kwamba wao walifuata taratibu zote kabla ya kuwahamisha wakazi hao ikiwa ni pamoja na kubandika notisi ya siku 44 kabla ya zoezi kufanyika

No comments: