Wednesday, November 18, 2015

SERIKALI YAJIPANGA KUKABILIANA NA WIZI WA UMEME NCHINI.

index
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi. Badra Masoud akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani)mapema leo jijini Dar es Salaam kuhusu mpango wa Serikali wa kuunda kikosi maalum cha kukabiliana na tatizo la wizi wa umeme na kuimarisha ukaguzi ili kubaini wateja wasio waaminifu na kuwachukulia hatua za kisheria. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na Fatma Salum- Maelezo)

…………………………………………………………………………..
Na. Fatma Salum – MAELEZO
Serikali inatarajia kuunda kikosi maalum kitakachojumuisha wataalam kutoka taasisi mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la wizi wa umeme linalopelekea Shirika la Umeme (TANESCO) kukosa mapato inavyostahili.
Hayo yamebainishwa na Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi. Badra Masoud wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Bi. Badra amesema kuwa kutokana na wizi wa umeme kukithiri na kuliingizia hasara Shirika la Umeme (TANESCO),
Wizara itaunda kikosi hicho kitakachojumuisha wataalam kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini na Vyombo vya Usalama ili kukabiliana na tatizo hilo. 
“Aidha Wizara ya Nishati na Madini imeliagiza shirika la TANESCO kuimarisha kikosi chake cha ukaguzi wa watumiaji wa umeme ili kubaini wateja wasio waaminifu wanaoiba umeme na kuwachukulia hatua za kisheria.” Alisema Badra.
Kwa upande mwingine Serikali imezitaka Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kuzingatia matumizi bora ya umeme ili kudhibiti upotevu wa nishati hiyo muhimu kwani imebainika kuwa kuna baadhi ya ofisi wana kawaida ya kuacha wazi vifaa vya umeme baada ya muda wa kazi vikiwemo vifaa kama kompyuta, AC na taa.
Aidha Bi. Badra ameongeza kuwa Serikali inatoa onyo kwa watu wanaohujumu miundombinu ya TANESCO ikiwemo kuchoma nguzo za umeme na kuiba mafuta ya transfoma kuacha mara moja kwani wakigundulika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumzia hali ya umeme nchini Bi. Badra amesema kuwa hali ni nzuri na hakuna mgawo wowote kwa sasa kwani kasi ya uzalishaji wa umeme ni nzuri na kiasi kinachopatikana sasa ni megawati 1500 huku matumizi yakiwa ni kati ya megawati 800 na 900 kwa siku.

No comments: