Monday, November 16, 2015

STARS KUWAVAA ALGERIA KESHO


Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, kitafanya mazoezi leo jioni saa 1 Algeria, sawa na saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Mustapher Tchaker utakaotumika kwa mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji Algeria.


Stars inayonolewa na kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa iliwasili salama jana jioni katika mji wa Blida, uliopo takribani kilometa 75 kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Houari Boumediene jijini Algiers.
Mkwasa amesema mchezo wa kesho watajituma kadri ya uwezo kuhakikisha wanapata ushindi, makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa awali yamefanyiwa kazi na anaamini vijana wake watapambana kusaka ushindi katika mchezo huo.
Wachezaji wote 21 wapo katika hali nzuri, hakuna mchezaj majeruhi hata mmoja, hivyo kocha Mkwasa ana wigo mpana wa kumtumia mchezaji yoyote anayemuhitaji kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.
Mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018, utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Mali na utaanza saa 1:15 usiku (Algeria) sawa na saa 3:15 usiku kwa saa nyumbani Tanzania na Afrika Mashariki.
KIBADENI ATANGAZA KILIMANJARO STARS
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania bara ‘Kilimanjaro Stars’, Abdallah Kibadeni ametangaza kikosi cha wachezaji 21 kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji itakayoanza kutimua vumbi Jumamosi Novemba 21, nchini Ethiopia.
Kibadeni anayesaidiwa na kocha msaidizi Juma Mgunda, amesema wachezaji aliowaita wapo katika hali nzuri na wamekua wakifanya mazoezi na kikosi cha Taifa Stars ambapo wao kama benchi la ufundi wamepata nafasi ya kuwa nao kwa muda mrefu na kutambua maendeleo yao.
“Tumechagua wachezaji kulingana na mahitaji ya timu, tumekua na wachezaji hawa kwa muda mrefu katika vipindi mbalimbali, tuna amini tuliowachagua watafanya vizuri katika michuano hiyo mikongwe barani Afrika” amesema Kibadeni.
Wachezaji walioitwa ni magolikipa, Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam), Said Mohamed (Mtibwa Sugar), walinzi Shomari Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa), Juma Abdul (Yanga) na Kelvin Yondani (Yanga).
Viungo Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Said Ndemla (Simba), Salum Telela (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Deus Kaseke (Yanga), washambuliaji John Bocco (Azam), Elias Maguri (Stand United), Ibrahim Hajibu (Simba), Malimi Busungu (Yanga) na Saimon Msuva (Yanga).
Michuano ya Kombe la Chalenji inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 21 na kumalizika Disemba 6, ambapo Kilimanjaro Stars imepangwa kundi A, lenye wenyeji Ethiopia, Rwanda na Somalia.
Wachezaji Said Mohamed, Juma Abdul, Hassan Kessy, Hassan Isihaka, Salum Abubakar na Ibrahim wanaendelea na mazoezi jijini Dar es salaam chini ya kocha msaidizi Juma Mgunda wakati wanawasubiri wachezaji wengine walioko nchini Algeria na kikosi cha Taifa Stars.
Kundi B lina Bingwa Mtetezi Kenya, Burundi, Uganda na Zanzibar, huku kundi C likiundwa na timu za Sudan, Sudani Kusini, Djibouti na waalikwa wa michuano hiyo timu ya taifa kutoka Malawi.

No comments: