Tuesday, November 10, 2015

Story Nne Mpya Kutoka TFF asubuhi hii zisikupite


KUZIONA STARS V ALGERIA 5000/=
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa Jumamosi kati ya Tanzania dhidi ya Algeria utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam bei ya chini kuwa ni shilingi elfu tano (5,000) tu.
Tiketi za mchezo huo zitaanzwa kuuzwa siku ya ijumaa katika vituo mbalimbali vinavyotumiwa na TFF kuuzia tiketi, ambapo kiingilio kingine kitakua ni elfu kumi (10,000) kwa viti vya VIP B & C, huku kiingilio cha elfu tano kikiwa ni kwa viti vya rangi ya Bluu, Kijani na rangi ya Machungwa.
Wakati huo huo kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhamininiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, kinatarajiwa kurejea nyumbani kesho Jumatano mchana kwa shirika la ndege la Fastjet tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Algeria siku ya Jumamosi.
Stars iliyoweka kambi nchini Afrika Kusini imekua ikifanya mazoezi kila siku katika uwanja wa Edenvale, ambapo mpaka sasa wachezaji wote wapo katika hali nzuri hakuna majeruhi na kila mmoja yupo tayari kwa mchezo wa Jumamosi.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema vijana wake wapo vizuri kifaya, kifikra na morali ni ya hali juu “wachezaji wamekua wakifanya mazoezi kwa nguvu na kuonyesha umakini mkubwa” alisema Mkwasa.
Aidha Mkwasa amewaomba watanzania na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti ya kuwashangilia vijana katika mchezo dhidi ya Algeria Jumamosi, kwani kutawafanya wachezaji kujisikia wapo nyumbani na kucheza kwa nguvu zaidi.
Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walioshinda kombe la Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa wiki na klabu yao ya TP Mazembe wanatarajiwa kuungana na wenzao kambini kesho jijini Dar ess alaam.

ALGERIA KUWASILI ALHAMISI
Msafara wa timu ya Taifa ya Algeria (The Desert Warriors) unatarajiwa kuwasili nchini siku ya Alhamis kwa ndege binafsi ya kukodi, ukiwa na jumla ya watu 65 wakiwamo wachezaji 24 tayari kwa mchezo wa Jumamosi Novemba 14 dhidi ya wenyeji Tanzania katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kocha mkuu wa timu hiyo Iitakayofikia hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Kempsinki, Christian Gourcuff raia wa Ufaransa ametaja kikosi cha wachezaji 24, wakiwemo wachezaji 18 wanaocheza katika klabu za Ulaya kwa ajili ya kuikabili Tanzania.
Wachezaji wanaotarajiwa kuwasili Alhamisi ni walinda mlango, Doukha Izeddine (JS Kabliye), M’bolhi Rais (Antalyaspor), Asselah Malik (CR Belouizdad), walinzi Zeffane Mehdi (Rennes), Medjani Carl (Trabzonspor), Ziti Mohamed (JS Kabliye), Mesbah Eddine (Sampordia), Bensebaini Ramy (Montpeller), Belkarou Hichem (Club African), Ghoulam Faouzi (Namples), Mandi Aissa (Reims).
Viungo ni Guedioura Adlane (Watford), Boudebouz Ryad (Montpeller), Taider Saphir (Bologna), Abeid Mehdi (Panathinacos), Bentaleb Nabil (Tottenham), Ghezzal Rachid (Lyon), Melsoub Walid (Lorient), Marhez Ryad (Leicester).
Washambuliaji  Benrhama Said (Nice), Sliman Islam (Sporting Lisbon), Belfodil Ishak (Beni Yas), Brahimi Yassine (FC Porto) na Bounedjah Baghdad (Etoile du Saleh)

KILIMANJARO YAPANGWA NA WENYEJI CECAFA
Ratiba ya michuano ya Kombe la Challenji kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenger Cup) imetoka jana ambapo timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Star’ imepangwa kundi moja na wenyeji Ethiopia.
Katika taarifa ya CECAFA iliyotolewa jana, Kilimanjaro Star imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Ethiopia, Somali na waaalikwa wa michuano hiyo timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’.
Kundi B lina  Bingwa mtetezi timu ya Kenya, Uganda, Burundi na Djibouti, huku kundi C likiwa na timu za Rwanda, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 21 nchini Ethiopia katika mji wa Addis Ababa na kumalizika Disemba 6 mwaka huu.

AZAMHD CUP KUENDELEA LEO
Michuano ya Kombe la Shirikisho (AzamHD Federation Cup) inatarajiwa kuendelea leo katika viwanja vinne tofauti nchini, ambapo kila timu inahitaji kupata ushindi ili kusonga mbele katika mzunguko wa pili utakaochezwa mwezi Disemba mwaka huu.

Jijini Mbeya wenyeji Mbeya Warriors watakuwa wenyeji wa Wenda FC mchezo utakaochezwa uwanja wa Sokoine jijini humo, huku katika uwanja wa Majimaji mjini Songera timu ya Mighty Elephant watakua wenyeji wa African Wanderes.
Kariakoo ya Lindi watawakaribisha Changanyikeni FC katika uwanja wa Ilulu, huku timu ya Sabasaba ya mjini Morogoro wakiwakaribisha jirani zao Mkamba Rangers katika uwanja wa Jamhuri.
Michuano hiyo itaendelea kesho Jumatano kwa michezo miwili, Polisi Morogoro watawakaribisha Green Warriors uwanja wa Jamhuri mjini humo, huku timu ya Mshikamano FC wakiwa wenyeji wa Cosmopolitan katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Katika michezo iliyochezwa jana, Abajalo ilibuka na ushindi wa mabao 5 – 1 dhidi ya Transit Camp, huku Pamba FC ya jijini Mwanza ikiibuka na ushindi wa bao 1- 10 dhidi ya Bulyankulu FC ya mkoani Shinyanga.

No comments: