Sunday, November 15, 2015

TATU BORA USPIKA CCM HAWA HAPA,SITTA ATUPWA NJE

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa NEC ,CCM Makao Makuu Dodoma akiwa ameshikilia kitabu cha Kanuni za Kamati ya Wabunge Wote wa Chama Cha Mapinduzi.

Kamati Kuu CCM imewapitisha Job Ndugai, Abdullah Ali Mwinyi na Dr. Tulia Ackson Mwansasu kugombea nafasi ya Uspika wa Bunge la 11.

Majina hayo yamepenya kutoka katika orodha ya majina 21, miongoni mwao akiwemo Spika wa Bunge la 9, Samuel Sitta, Dkt. Didas Masaburi ambaye alitangaza kujitoa katika dakika za mwisho, Dkt Kalokola na wengineo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jioni ya leo baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichoongozwa na mwenyekiti wake Dkt Jakaya Kikwete mjini Dodoma, jina moja kati ya hayo matatu litatangazwa kesho Jumatatu ikiwa ni pamoja na jina la mgombea wa nafasi ya Naibu Spika.

Katika waliopitishwa: 
Job Ndugai ni mbunge mteule jimbo la Kongwa Dodoma na pia alikuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita.
Dkt Tulia Ackson(PICHANI JUU) ni Naibu Mwanasheria mkuu wa serikali, pia alikuwa ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba akitokea taasisi za elimu ya juu. Amekuwa mhadhiri wa sheria katika kitivo (sasa shule) cha sheria chuo kikuu cha Dar es salaam.
Abdullah Mwinyi ni mtoto wa Rais mstaafu Al Hajj Aly Hassan Mwinyi na ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Je, Nani kati ya hawa watatu apewe nafasi na CCM?

No comments: