Tuesday, November 10, 2015

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YAVISHUKURU VYOMBO VYA HABARI

  Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Giveness Aswile, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuvishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti vizuri katika kipindi chote cha uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa NEC, Emanuel Kavishe.PICHA  NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG.
……………………………………………………………………………

Lilian Lundo-MAELEZO
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa mafanikio ya asilimia 80 ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yametokana na ushiriki mkubwa wa vyombo vya habari vilivyotekeleza kwa ufanisi kazi ya kuelimisha na kutoa habari kuhusu uchaguzi huo.
Akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa tume hiyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Giveness Aswile, amevishukuru vyombo vya habari kutokana na kazi hiyo katika kipindi chote cha uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
Alisema amani ya Tanzania iliendelea kuimarika katika kipindi chote cha uchaguzi kwa sababu vyombo vya habari vilisimamia na kutetea haki za wananchi.
Aliongeza kuwa hata tume ilifanya kazi kwa urahisi kutokana na kazi kubwa ya uelimishaji iliyofanywa na vyombo vya habari, hivyo kuipunguzia kazi NEC ya kuwaelimisha wananchi juu ya mambo ya msingi ya uchaguzi mkuu.
 “Amani ya nchi hii ilisimama kwa sababu vyombo vya habari vilisimama kutetea wananchi na tume, ilifika mahali maswali kutoka kwa wananchi yalipungua kutokana na maswali mengi kujibiwa kupitia vyombo vya habari” Alisema Giveness.
Naye Mkurugenzi Idara ya Sheria wa tume hiyo, Emmanuel Kawishe alisema hakuwa na ufahamu sahihi kuhusu vyombo vya habari na umuhimu wake katika kutekeleza majukumu yake  kwa wananchi.
 “Zamani nilifahamu mwanahabari ni adui kumbe ni daraja kati ya mtoa habari na mpokea habari, katika zoezi zima la uchaguzi mkuu wanahabari walikuwa ni sehemu ya waliotoa elimu ya mpiga kura wameweza kutumia kalamu zao vizuri.” Alisema Bwana Kawishe
Alifafanua kuwa wanahabari walifanya kazi yao kwa kuzingazitia maadili ya kazi yao kwa kutofungamana na upande wowote na kuitangaza tume kwa mtazamo chanya kwa wananchi.
Kawishe alisema kuwa vyombo vimeweza kuitangaza vizuri tume kwani kila alipopita wananchi wamekuwa wakiipongeza NEC kwa kazi nzuri ya utoaji wa elimu ya mpiga kura katika vyombo vya habari.
Uchaguzi Mkuu wa mwak 2015, umeshuhudia ushirikishwaji mkubwa wa vyombo vya habari ambapo vyombo vya habari vilipewa nafasi kubwa ya kutoa habari kuhusu uchaguzi huo ikiwemo kutoa vitambulisho vilivyowaruhusu waandishi wa habari kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.

No comments: