Friday, December 18, 2015

Wakosa Maji safi na salama kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Mkazi wa Ndanda Akitoka Kutafuta maji ambayo yamekuwa adimu kwa miaka mingi katika maeneo hayo
Haika Kimaro
Masasi.Wananchii wa Jimbo la Ndanda Wilaya ya Masasi wameendelea kulalamikia tatizo la Upatikanaji wa maji safi na salama jambo linalopeleka kutembea umbali wa Zaidi ya Kilomita Kumi kutafuta maji kwenye bwala la Demuni  ambayo nayo sio salama kwa matumizi kutokana na kutumika na kila mtu.

Changamoto hiyo ya maji imekuwa ya muda mrefu na kuonekana kushindwa kutatuliwa na viongozi wa serikali licha ya tatizo hilo kujulikana.

Wakizungumza na mtandao huu wamesema kuwa bwawa hilo linatumika kwa Vijiji 5 vya Wilaya ya masasi jimbo la Ndanda ambavyo ni Lukuledi A Na B Mpanyani,Mkolopola pamoja na Mraushi ambavyo vyote vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa Maji safi na Salama jambo linaloathiri wakazi wa vijiji hivyo kwa kipindi kirefu ingawa wananunua maji hayo kwa shilingi 500 yenye ujazo wa Lita 20
Mbunge wa Ndanda CECIL MWAMBE akiongea na wananchi wanaochota maji katika Bwawa la Demuni kata ya Lukuledi(Picha na Haika Kimaro)
Raymond Mbalale anasema tatizo hilo linaonekana kuzoeleka sasa kutokana  kushindwa kufanyiwa kazi lakini pia zahanati ya eneo hilo inaonekana kuathirika kutokana  na kukosa maji safi na salama na kutegemea maji ya Mvua ambayo yanapatikana kwa Msimu.

“Wananchi tunakabiliwa na kero kubwa ya maji ambayo imekuwa ikitulazimu kutumia muda mwingi kwenda umbali mrefu kutafuta maji..kama mnavyoona hapa hata zahanati yetu haifanyi vizuri kutokana na ukosefu wa maji,:alisema Mbalale
Wananchi wakichota maji katika Bwawa la Demunu
Naye Amina Mrope alisema tatizo hilo pia limekuwa likichangia migogoro katika ndoa kutokana na kutumia muda mwingi kusaka maji na kuacha kuhudumia family.
“Muda mwingi tunautumia kusaka maji tunashindwa kuhudumia familia zetu watoto wetu wanashinda njaa tunapoenda kutafuta maji na wakati mwingine ukirudi nyumbani unakuta mume amenua,tunaiomba serikali itutatulie kero hii ya tangu uhuru,”alisema Mrope

Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe  alitembelea eneo la bwawa na kujionea uharibifu wa mazingira na kuahidi kufanyia kazi kwa kujenga mabomba ya kuvuta maji ili kuepuka wananchi kuingia ndani ya maji na Kuchafua zaidi.

“Changamoto ya maji naitambua ni ya muda mtefu lakini nitashirikiana na wananchi kuona ni kwa namna gani tunamaliza tatizo hili lakini muhimu ni wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya maji pale itakapokuwepo ili kuondokana na kero hii,”alisema Mwambe

Hata hivyo changamoto hii ya maji kwa kiasi kikubwa imeathiri zahanati hii ya kijiji ambapo wagonjwa wanalazimika kutumia maji ambayo sio salama lakini pia vijiji vitano vianvyozunguka bwawa hili vinatumia maji haya swala ambalo serikali inapaswa kulifanyia kazi kwa haraka zaidi ili wanananchii wake wapate maji safi na salama.

No comments: