Mabadilikoo--Tizama Mradi wa kwanza wa Meya mpya wa Kinondoni.


Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mh. Boniface Jacob akisikiliza maswali ya wanahabari (hawapo pichani) juu ya mradi huo utakavyosaidia Manispaa ya Kinondoni ikiwemo suala hilo la usafi. Kushoto ni Florian Koelesch mshauri mtaalam wa mpango huo kutoka Ujerumani.


Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mh. Boniface Jacob (katikati) akizungumza katika mkutano maalum juu ya ushirikiano baina ya Manispaa hiyo ya Kinondoni na jiji la Hamburg la nchini Ujerumani watakavyojenga dampo la kisasa huko katika eneo la Mabwepande. Kushoto ni Florian Koelesch mshauri mtaalam wa mpango huo kutoka Ujerumani. Wengine ni watendaji wa Manispaa hiyo. (Picha zote na Andrew Chale,modewjiblog).Manispaa ya Kinondoni kwa ushirikiano na Manispaa ya Jiji la Hamburg, nchini Ujerumani ziko katika hatua za mwisho za ujenzi wa mradi mkubwa kwa ajili ya kukusanya taka zinazooza na kuzizalisha kuwa mbolea ambao utagharimu Euro Mil. 1.6 ambazo ni sawa na Shilingi bil. 3.5 utakapokuwa umekamilika na kuanza kazi ifikapo Juni mwakani.


Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo baada ya kumkaribisha ofisini kwake Mwakilishi wa Jiji la Hamburg ambaye pia Mtaalam Mshauri wa Mradi huo, Dkt. Florian Koelsch, Meya Jacob amesema kuwa baada ya mradi kukamilika kutakuwa na uhakika wa kukusanya na kuzoa nusu ya taka zote zinazozalishwa kwa siku katika manispaa hiyo ambazo kwa sasa zinakadiriwa kuwa tani 2,026.

Meya Jacob amesema kuwa ujenzi wa mradi huo utakaoanza na kuweka mitambo yake (compost plant) itakayokuwa ikibadilisha taka zinazooza kuwa mbolea, utaanza mwezi mmoja ujao katika eneo la Mabwepande, jijini Dar es Salaam, 
Amesema kuwa mradi huo unaanza kutekelezwa siku chache baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, akiongeza kuwa manispaa hizo mbili ambazo ziko katika ushirikiano zilipeana majukumu ya kufanya ambapo Jiji la Hamburg walikubali kufadhili ujenzi na usimamizi kwa mwaka mmoja utakapokuwa umekamilika na Manispaa ya Kinondoni ilipewa jukumu la kutafuta ardhi ya kujenga mitambo hiyo.

“Tayari tumepata ardhi takriban ekari 20 katika Kata ya Mabwepande. Kazi ya ujenzi itaanza mwezi mmoja ujao kwa maana ya kufunga mitambo, inakadiriwa ndani ya mwaka mmoja hadi Juni mwakani mradi utakuwa tayari unaanza kazi. Kwa upande wetu kwa kweli tuko tayari,” amesema Meya Jacob.

Meya Jacob amesema kuwa yeye pamoja na baraza la madiwani analoliongoza kwa kushirikiana na watendaji, wamejipanga kikamilifu kuwatumikia wananchi kwa kuzifanyia kazi kero mbalimbali, likiwemo suala la kuhakikisha manispaa inakuwa safi kimazingira.

“Tumejipanga ipasavyo…tunataka uchafu uwe mahali panapostahili ama kwa kuzalishwa kuwa mbolea ua kuchomwa moto. Nashukuru tangu nimeingia tunaendelea kupata uungwaji mkono wa wadau mbalimbali. Kuna mpango mwingine wa kuwa na dampo la kuchoma taka, dampo tanuru. Ukikamilika pia tutawataarifu,” ameongeza Meya Jacob.

Amesema kuwa kwa sasa Manispaa ya Kinondoni inazalisha taka takriban tani 2,026 kila siku kutokana na shughuli za mtu mmoja mmoja (majumbani) na katika taasisi kv; masoko, shule n.k, ambapo kwa sasa manispaa hiyo ina uwezo wa kukusanya na kuzoa robo ya taka hizo huku changamoto ya kumaliza kero hiyo ikiwa bado ni kubwa ndiyo maana kupitia uongozi wake wanabuni miradi mbalimbali kupata suluhisho la uhakika kusafisha manispaa hiyo.

Kwa upande Dkt. Koelsch amesema kuwa Jiji la Hamburg litafurahi iwapo mradi huo utaanza haraka iwezekanavyo kabla mwaka wa fedha wa bajeti ya Ujerumani haujaisha. 
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya ushirikiano wa pande zote hizo mbili ambao anatarajiwa utaendelea kuimarishwa kwa manufaa na maslahi ya wananchi wa nchi zote mbili.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.