Thursday, January 28, 2016

SERIKALI YAENDELEA KUREJESHA MALI ZILIZOPATIKANA NA UHUJUMU UCHUMI

DI1
Mkurugenzi wa upelelezi Jeshi la Polisi Kamishina Diwani Athumani akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa mkutano wa kuelezea mikakati na malengo ya Serikali katika kupamabana na kudhibiti wahalifu wa kuhujumu uchumi uliofanyika leo jijini Dar  es salaam.
DI2
Mkurugenzi wa Upelelezi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) Bw. Alex Mufungo akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa mkutano wa kuelezea mikakati na malengo ya Serikali katika kupamabana na kudhibiti wahalifu wa kuhujumu uchumi uliofanyika leo jijini Dar  es salaam pembeni yake ni Mkurugenzi wa mashitaka nchini DPP Biswalo Mganga.
DI3
Waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Kamishina Diwani Athuman hayupo pichani wakati wa mkutano wa kuelezea mikakati na malengo ya Serikali katika kupamabana na kudhibiti wahalifu wa kuhujumu uchumi uliofanyika leo jijini Dar  es salaam.
Picha zote na Ally Daud -MAELEZO
………………………………………………………………………………………………………
NA MAGRETH KINABO NA ALLY DAUD – MAELEZO
Serikali inaendelea kusimamia urejeshaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya kihalifu kupitia mpango wa kupambana na uhalifu ulioanzishwa mwaka 2012 kwa kuwashtaki na kuwataifishia mali zao pindi upelelezi ukikamilika na kubainika mhalifu ana makosa hayo.
Baadhi ya watuhumiwa kadhaa wamepelewa mahakamani na kufungwa, ikiwemo mali zao kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Hayo yalisemwa na  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) Biswalo Mganga wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo kwenye ofiisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi   jijini Dar es salaam, ambapo  alisema kuwa hatua hizo zimechukuliwa mara baada ya  upelelezi wa makosa ya kuhujumu uchumi kukamilika na kumbaini mhusika.
Aidha Mganga aliongeza kwamba  mhusika  hushtakiwa na mali zake kutaifishwa kulingana na kosa lake, pia suala hili litamgusa kila mtu, wakiwemo  watumishi wa umma.
“Mhalifu wa kuhujumu uchumi wa nchi ikiwemo usafirishaji wa nyara za Serikali, uuzaji wa madawa ya kulevya na kujipatia mali kwa njia ya rushwa watatumikia adhabu ya kulipa faini, kufungwa jela na kutaifishiwa mali zake pindi atapobainika na makosa hayo” alisema  Mganga.
Alisema kufuatia mkakati huo, Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa kesi 23 ambazo ziliwasilishwa kwa DPP na kati ya hizo tatu (3) zimetolewa uamuzi na nyingine ishirini (20) ziko katika hatua ya maombi ya kupata amri ya mahakama ili ziweze kuziwa au kutaifishwa.
Alizitaja baadhi ya kesi za dawa za kulevya ambazo zimefikia ukomo na kutolewa uamuzi Januari 27, mwaka huu.
Mkoani Kilimanjaro kesi mojawapo ni Josephine Waizela, ambaye ni raia wa Kenya aliyetiwa hatiani  kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine  zenye uzito wa kilogram tatu zikiwa na thamani ya Sh. Milioni 162 na kufungwa kifungo cha maisha.
Kesi nyingine ni namba 46 ya mwaka 2014 kutoka pia mkoani Kilimanjaro ambayo ilihusisha watu watatu, mmoja kati yao ambaye ni Hamis Mbwana alitiwa hatiani kwa kukutwa na dawa za kulevya aina Heroine zenye uzito wa gram 3191.11 na thamani ya Sh. Milioni 143, watuhumiwa wengine wawili katika kesi hiyo waliachiwa huru.
Mganga alizitaja baadhi ya kesi nyingine za uhujumu uchumi ni namba 6 ya mwaka 2015, ilisikilizwa mkoani Mbeya ambayo iliwahusisha raia wanne kutoka nchini China waliotiwa hatiani kwa kosa la kukutwa meno ya vifaru 11. Raia hao ni  Song Lei , Xiao Shaodan, Chen Jianlin na HU Liang, ambao wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 na kulipa faini ya Sh. Milioni 9,288 kwa kila mmoja.
Kesi nyingine  ya uhujumu uchumi namba 3 ya mwaka 2016 iliyomhusisha raia wa Tanzania Amani Rashid Ngaza aliyetiwa hatiani  kwa  kosa la kukutwa na meno ya tembo nane iliyosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Katavi, wilaya ya Mpanda. Mtuhumiwa huyo amefungwa kifungo cha miaka 30 na kullipa faini ya Sh. bilioni 1.2.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Maganga alibainisha baadhi ya mali zilizotaifishwa kutoka kwa wananchi kuwa ni magari matano aina ya Toyota Rv 4 mbili ,Suzuki, Toyota Surf , Hiace pamoja na nyumba  kutoka kwa washtakiwa mbalimbali wa makosa ya kuhujumu uchumi.
Aidha,  Mganga alitoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano bila uwoga katika kufichua mali za mafisadi ili sheria ichukue mkondo wake pamoja na kuwataka wananchi wasijihusishe kwa njia yoyote ile ili kuficha umiliki wa mali ya mtu mwingine aliyoipata kiharamu kwa nia ya kuficha uhalifu wake kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
“Kwa mujibu wa Sheria aliyeshirikikuficha mali ya mtu mwingine inayohusiana na uhalifukwa njia yoyote ile pia anaweza kushitakiwa kama aliyetenda kosa la ufisadi,” alisema.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Kamishna Diwani Athumani alisema kuwa atakayekamatwa na kosa la wizi au mali ya haramu atatumikia adhabu na mali zake kutaifishwa.
“Mhalifu akibainika na mshataka ya wizi au kujipatia mali kwa njia ya haramu atatumikia adhabu na kutaifishiwa mali zake kama vile magari, nyumba, boti, viwanja na fedha taslimu” alisema Kamishna Athumani.
Aidha, Kamishna Athumani aliongeza kuwa uzoefu wao unawaonyesha kwamba wahalifu wanatumia majina ya wake zao, waume zao, watoto wao na wakati mwingine kutumia majina ya watu ambao hawapo ili kuendelea kufaidika na mali walizozipata kwa niia za uhalifu.
“Hakuna mhalifu atakayepona katika mapambano haya pia uhalifu haulipi na hauna nafasi nchini” alisistiza Kamishina Athuman.
Mbali na hayo, Mkurugenzi wa upelelezi Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) Alex Mfungo pia alisema kuwa wameanzisha kitengo cha kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu ikiwemo rushwa.
Tangu mwaka 1990, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitambua utaifishaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya kihalifu kama kipaumbele katika mfumo wa haki jinai wa kupigana na uhalifu.  Haisadii sana katika jitihada za kupambana na uhalifu ikiwa mhalifu atapata adhabu ama ya kutozwa faini au kwenda jela ikiwa ataachiwa uhuru na kupewa fursa ya kutumia fedha au mali iliyopatikana kwa uhalifu huo.
Zaidi, fedha zilizoibwa na wanasiasa wala rushwa pamoja na wahalifu wengine, zinahitaji kutaifishwa na kuelekezwa katika maeneo muhimu yenye mahitaji.
Sheria ya Utaifishaji wa Mali Haramu ilipitishwa na Bunge mwaka 1991 ili kuendana na muelekeo wa Kimataifa pamoja na mikataba ya Kimataifa ambayo imeridhiwa na nchi yetu

No comments: