Tuesday, January 26, 2016

STORY TATU ZA KIMICHEZO LEO TANZANIA

MWESIGWA AFUNGUA KOZI YA NGAZI YA JUU KWA WANAWAKE

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine leo amefungua kozi ya ngazi ya juu ya ukocha kwa wanawake (High Level Coaching Course) iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo, Mwesigwa amewataka washiriki wa kozi hiyo kuzingatia mafunzo hayo na kuitumia vyema fursa hiyo adimu waliyoipata.
Mwesigwa amewataka washiriki kuhakikisha kozi hiyo ya siku tano, inawasaidia na kwenda kuwa walimu wa mpira wa miguu kwa wanawake, na kuongeza mwamko kwa wanawake wengi kuupenda na kuucheza mpira wa miguu.
Aidha Mwesigwa, amewataka washiriki wa kozi hiyo kuzingatia maelekezo ya mkufunzi, nidhamu ya ndani na nje ya uwanja kwani imekua ni bahati nzuri kwao kupata nafasi ya kushiriki kozi hiyo ya ngazi ya juu.
Naye mkufunzi wa kozi hiyo anayetambulika na FIFA/CAF, Sunday Kayuni amesema atatumia uwezo wake wote kuhakikisha washiriki wa kozi hiyo wanajifunza na kuelewa vizuri mafunzo yake, ili waweze kuwa walimu wazuri watakapokwenda kuanza kufundisha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake ya TFF, Amina Karuma ameishukuru TFF kwa kuendesha kozi hiyo  na kusema kupatikana waalimu wengi wa kike kutaongeza mwamko wa wanawake kuucheza mpira wa miguu.

Jumla ya washiriki 25 wanashiriki kozi hiyo kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao ni Fatuma Omary, Esther Chabruma, AMina Mwinchum, Sweetie Charles, Pendo John, Berlina Mwaipungu, Mariam Mchaina, Elizabeth Sokoni, Sophia Mkumba, Marry Masatu, Aziza Mbwele, Fadhila Yusuph.
Wengine ni Veneranda Mbano, Mariam Aziz, Hilda Masanche, Chichi Mwidege, Sophia Edward, Asha Rashid, Fatuma Khatibu, Neema Sanga, Hindu Muharami, Tatu Malogo, Komba Alfred, Veroinca Ngonyani, Judith nyatto na Ingfridy Kimaro.

AZAM, SIMBA, YANGA ZAFUZU 16

Timu za Azam FC, Simba SC, Yanga zimeungana na timu zingine saba kufuzu kwa hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mzunguko wa nne utakaochezwa mwishoni mwa mwezi Februari, huku michezo mine ikichezwa leo katika viwanja mbalimbali nchini.
Jumla ya michezo 10 mpaka sasa imeshachezwa na timu kumi kujikatia tiketi ya kucheza mzunguko wa nne, ambao utazikutanisha jumla ya timu 16 mwezi ujao kusaka timu nane zitakazosonga mbele hatua ya nane bora (Robo Fainali).
Timu zilizofuzu hatua ya 16 bora mpaka sasa ni Azam FC, JKT Mlale, Mwadui FC, Ndanda FC, Panone FC, Rhino Rangers, Simba SC, Tanzania Prisons, Toto Africans na Young Africans.
Leo michezo minne itachezwa, Mtibwa Sugar v Abajalo (Jamhuri – Morogoro), Geita Gold v Mgambo Shooting (Nyankumbu – Geita), Lipuli FC v JKT Ruvu (Wambi – Mafinga), na African Sports v Coastal Union (Mkwakwani – Tanga).
Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mwaka huu, ataiwakilisha Tanzania mwaka 2017 kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF-CC)

TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA KOCHA MINGANGE

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetuma salamu za rambirambi kwa Kocha Mkuu wa klabu ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom, Meja Mstaafu Abdul Mingange kufuatia kifo cha mke wake Fatma Juma kilichotokea mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.
Katika salamu zake kwenda kwa familia ya marehemu, TFF imempa pole mme wa marehemu Meja Mingange, ndugu jamaa, marafiki pamoja na klabu ya Mbeya City kufuatia kifo hicho.
Mazishi ya marehemu Fatma Juma yamefanyika Jumapili iliyopita katika makaburi ya Matombo mkoani Morogoro

No comments: