Monday, January 18, 2016

Taarifa mbalimbali kutoka Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam

WATUHUMIWA SUGU WA DAWA ZA KULEVYA KUFIKISHWA MAHAKAMANI



 Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa kuuza madawa ya kulevya hapa nchini. Watuhumiwa hawa ni miongoni mwa wauza madawa wazoefu na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kujibu mashtaka yanayowakabili.
Watuhumiwa hao walikamatwa na kilogram 09 za madawa ya kulevya aina ya HEROINE kutoka nchini Pakistan mwaka 2015 ni kama ifuatavyo:

1.    MOHAMED S/O ABDALLA OMARI, Miaka 37, mfanyabiashara, mkazi wa Tegeta Nyuki, anatuhumiwa kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu. Anatuhumiwa kumsafirisha MWINYI S/O MGOBANYA, Mkazi wa Ununio na kumweka rehani (bond) huko Pakistan kisha akachukua madawa ya kulevya kwa mali kauli.


2.   NASSORO S/O SULEIMAN, Miaka 35, meneja wa TUNGWE BUREAU DE CHANGE katika jengo la IPS jijini Dar es Salaam anatuhumiwa kwa kosa la kushirikiana na genge la wauzaji wa madawa ya kulevya na kusafirisha kiasi kikubwa cha pesa kwa njia ambazo sio rasmi.

Mtuhumiwa wingine DAUD S/O AYUBU ADAM @ KANYAU, Miaka 46, Mfanyabiashara mkazi wa Salasala jiji Dar es Salaam na Kibaha. Anatuhumiwa kusafirisha madawa ya kulevya lakini hatafikishwa mahakamani kwa kuwa uchunguzi dhidi yake bado unaendelea.
Takwimu zinaonyesha kuwa Mwaka 2014 kiasi cha kilogram 304.61 za HEROINE na kilogram 29.68 za COCAINE kilikamatwa na watuhumiwa 14501 ambapo miongoni mwao watanzania walikuwa 14467 ikilinganishwa na mwaka 2010 ambapo zilikamatwa kilogram 123 za HEROINE na kilogram 16.74 za COCAINE na watuhumiwa 23 walikamatwa watanzania wakiwa 22
Uchunguzi umebaini kuwa sababu kuu ya ongezeko la takwimu hizi ni kushamiri kwa mitandao ya wahalifu wa kimataifa wa madawa ya kulevya wanaoshirikiana na watanzania kufanya biashara ya kusafirisha binadamu kwenda nchi wazalishaji wa madawa ya kulevya katika nchi za kiarabu na kuwaweka rehani ili wapatiwe kiasi kikubwa cha madawa kwa mali kauli.
Hatima ya watanzania wanaowekwa rehani ni kupigwa mijeredi kwa nyaya za umeme, na wakati mwingine kuuawa ili hali wale waliowapeleka huko huendelea kujineemesha.
Kutokana na tathmini hiyo, Jeshi la Polisi tumeanzisha mikakati inayolenga kusambaratisha mitandao ya magenge ya uhalifu yanayofanya uhalifu hapa nchini na nje ya nchi za nje ili kupunguza au kuzuia uingizwaji wa madawa ya kulevya.

KUPATIKANA KWA SILAHA INAYOMILIKIWA KIHALALI.
Tarehe 09/01/2016 jeshi la polisi liliwakamatwa watuhumiwa wawili JACKSON S/O JUMANNE, miaka 18, mfanyakazi wa ndani, mkazi wa Bunju “A”, na DEOGRATIAS S/O PAMBO kwa tuhuma za kuiba silaha Bastola aina ya COMPAQ CZ75D yenye namba TZCAR 100416 iliyotengenezwa Jamhuri ya CZECH. Hii ni baada ya mlalamikaji SAMWELI S/O SAMWANG’OMBI, Mkazi wa Bunju, Kinondoni jijini Dar es Salaam kutoa taarifa polisi kwamba ameibiwa silaha hiyo.
Watuhumiwa walipohojiwa walikiri kuiba silaha hiyo na kueleza walipoifisha huko maeneo ya Mtoni kwa Azizi Ally. Ufuatiliaji uliendelea ndipo alipokamatwa mtuhumiwa mwingine kwa jina la JOHN S/O SAMSON MZEZE, miaka 24, mfanyabiashara, mkazi wa kambi ya polisi kilwa road. ambaye alieleza kuwa siku ya tukio kuna kijana alifika katika eneo lake la biashara huko mtoni kwa Azizi Ally na kununua soda. Baadaye kijana huyo alimtishia JOHN SAMSON MZEZE kwa bastola ili atoe fedha lakini alipambana nae kwa kushirikiana na wananchi ndipo mhalifu huyo alipotelekeza silaha hiyo na kukimbia. JOHN SAMSON MZEZE na wenzake waliisalimisha silaha hiyo kityuo cha polisi Kilwa road

WAHALIFU SUGU 06 WA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA WAKAMATWA
       Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 06 kwa tuhuma za kujihusisha na unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji na mikoa ya jirani. Watuhumiwa hao wamekamatwa tarehe 11/01/2016 na 16/01/2016 katika maeneo tofauti kufuatia taarifa za raia wema ambao ni wazalendo kwa nchi yao.
Watuhumiwa hawa wamehojiwa na kukiri kuhusika katika baadhi ya matukio ya uporaji wa kutumia silaha jijini Dar es Salaam na kwamba baadhi ya wenzao wamefungwa gerezani kutumikia adhabu kwa makosa kama haya. Watuhumiwa hao ni kama ifuatavyo:
1.    AGASESE S/O MALA, Miaka 40, Mkazi wa Mbagala Chamazi
2.   ABDALLAH S/O JUMA, Miaka 32, Mkazi wa Tandika.
3.   KRISTAN S/O NYONI, Miaka 28, Mkazi wa Mbagala Charambe.
4.   VICTOR S/O GABRIEL, Miaka ? Mkazi wa Gongolamboto
5.   PROSPER S/O GERVAS KALALA @ CHIEF, Miaka 41, Mkazi wa Yombo Kipera
6.   MOHAMED S/O ABDUL @ MUD, Miaka 23, Mkazi wa Yombo Buza.
Upelelezi juu ya watuhumiwa hawa unaendelea na utakapokamilika jalada la kesi litapelekwa kwa mwanasheria wa Serikali kwa hatua zake muhimu.

KUKAMATWA KWA MAGARI YA WIZI PAMOJA NA WATUHUMIWA
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata magari yaliyokuwa yameibwa maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam na mikoani pamoja na watuhumiwa.
1.    Gari na. T271 DCT, Toyota IST, rangi nyeusi imekamatwa huko Mbeya akiwanayo mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari anayeitwa ROBINSON S/O SAMWELI, Mkazi wa Mwanjelwa na Sai mkoani Mbeya. Gari hili lilibiwa nyumbani kwa Dr.REGINARD huko  Kimara, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

2.   Gari na. T916 DCL, aina ya Mitsubishi FUSO ambalo liliibwa maeneo ya Kimara na kukamatwa huko Tegeta Masaiti nyumbani kwa HASSAN S/O PHILIPO MAZWAZWA ambaye ni mwizi sugu wa magari ambaye anatafutwa. Gari hilo lilikuwa limebadilishwa baadhi ya vitu ikiwa ni pamoja na kupigwa rangi nyingine

3.   Gari na. T593 CEL, aina ya Toyota Prado iliibiwa huko Regency Estate

4.   T.999 DDB, aina ya Toyota Prado, iliyoibwa katika maegesho ya Regency Estate ilikamatwa huko Gezaulole nyumbani kwa mtu.  

TAARIFA ZA USALAMA BARABARANI KANDA MAALUM
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam kimeendelea kufanya oparesheni ilianza tarehe 02/01/2016 hadi sasa ili kuhakikisha madereva wote wa vyombo vya moto wanazingatia na kufuata sheria za usalama barabarani muda wote.
Oparesheni hiyo ililenga kutoa elimu kwa madereva na kuwakamata wale wanakaidi maelekezo yanayotolewa juu ya matumizi sahihi ya alama za barabarani na sheria za usalama barabarani. Pia magari, pikipiki, na bajaji vilikaguliwa kujua uhalali wake wa kuwa barabarani. Makosa yaliyokamatwa ni pamoja na matumizi mabaya ya barabara, ulevi, kukatisha route, kutotii amri, ubovu wa magari na makosa mengineyo.
Katika oparesheni hiyo jumla ya magari na pikipiki zilizokamatwa ni 24,068 na kutozwa faini ya jumla TSHS 722,040,000/= (Millioni mia saba ishirini na mbili, arobaini elfu tu).
Aidha, lengo ya Jeshi la Polisi si kukusanya kiasi kikubwa cha fedha bali kuona watanzania wanazingatia na kutii sheria za usalama barabarani wakati wote wanapokuwa na vyombo vya moto.

S. N. SIRRO - DCP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

No comments: