Saturday, February 6, 2016

Ijue sheria--Je unajua nini maana ya talaka na wakati gani unaweza kumpa mwenzio Talaka-sheria inasema hivyo



Kila itakapofika mwisho wa wiki msomaji wetu tutakupa makala mbalimbali za kisheria,kiafya na nyingine za kijamii ili kukusaidia kujua mambo mbalimbali ambayo tunaamini watanzania wengi hatuyajui lakini tunahitajika kuyafahamu.
Leo tumeanza kukupa baadhi ya mambo muhimu yanayopatikana katika sheria ya ndoa ya nchini Tanzania The Law of Marriage Act 1971 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.Na leo tutaangalia swala la talaka limekaaje kisheria 

Talaka kisheria
Neno talaka linaweza kuwa mojawapo ya maneno yaliyozoeleka midomoni au masikioni mwa watu wengi katika ulimwengu wa sasa.
Kwa lugha nyepesi, talaka ni kitendo cha wanandoa kuachana na mahusiano ya kindoa yaliyokuwa baina yao.



Lakini kisheria, ingawa maana ya talaka inaakisiwa na maana hii ya Kiswahili, lakini katika maana ya sheria kuna mambo mengine zaidi ya kuzingatia.
Tafsiri ya sheria ya ndoa ya Tanzania, sura ya 29 ya marekebisho ya sheria ya mwaka 2002, talaka ni kitendo cha mahakama yenye mamlaka katika shauri linalohusika, kutoa tamko la kuivunja ndoa iliyokuwapo,kwa sababu mbalimbali.



Hivyo, tukiangalia kwa mtazamo wa kihistoria, ndoa kwa mujibu wa sheria ya Kiingereza (common law) ambayo imeakisiwa sana na sheria ya ndoa ya Tanzania, ilikuwa haitambui sababu ya aina yeyote katika kuivunja ndoa kwa msingi wa talaka.



Lakini baada ya miaka mingi kupita, sheria ya talaka ilianza kutumika nchini Uingereza baada ya sababu kadhaa za kisheria za kuvunja ndoa kwa talaka kuanzishwa.
Sheria ya Talaka (The Divorce Act) ya mwaka 1969 ilianzishwa nchini Uingereza kufuatia ripoti ya askofu Kent wa nchini humo.



Mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 1969 serikali ya Tanzania kupitia tamko la serikali (Government Notice) namba 1 ya mwaka huo, iliyojulikana kama White Paper ilichukua msimamo na mtazamo huu wa sheria ya Kiingereza juu ya talaka.



Hadi mwaka 1971 tulipochukua msimamo huu wa sheria ya Uingereza juu ya talaka, mabadiliko makubwa ya kimsingi ya sheria juu ya talaka yalitokea katika sheria yetu hapa nchini nayo ni pamoja na kuwa na sababu moja tu inayoweza kuifanya ndoa kuvunjwa na mahakama kwa tamko la talaka, sababu hiyo ni kuwa mahakama itakapothibitisha kwamba ndoa hiyo imevunjika kabisa na haiwezi kurekebishika kutokana na kasoro zisizo weza kurekebishika.



Hivyo, sheria ya Tanzania katika hili nayo ikachukua sababu moja inayoweza kuifanya ndoa kuvunjwa na talaka.



Hata hivyo, wakati tunaangalia sheria hii, tunatakiwa kujua kwamba sababu moja ya kuivunja ndoa kwa talaka ipo Tanzania bara pekee.
Baadhi ya watu wanadhani sababu za kuvunja ndoa ni zile zinazoelezewa na sheria hii kama hali au mazingira ya kuthibitisha kwamba ndoa hiyo ina tofauti zisizorekebishika.



Sababu hizo ni pamoja na uzinifu nje ya ndoa, ukatili pamoja na kumkimbia/kumtelekeza mwanandoa mwezako.



Uzinifu ni mojawapo ya sababu zinazoipa mahakama mamlaka kisheria kuivunja ndoa yoyote.
Hata hivyo, unatakiwa kujua uzinifu una maana nyingi kutegemea na eneo husika.
Kimsingi uzinifu ni kitendo cha mwanandoa mmoja kufanya ngono nje ya mahusiano yake ya ndoa iliyo halalishwa.



Hapa katika kuondokana na wasiawasi wa kuweza kushindwa kuthibitisha uzinifu, sheria imetoa dhana kwamba pale tu itakapokutwa mume na mke wamelala pamoja na wako watupu, basi dhana hapa ni kwamba wametoka au wanataka kufanya ngono.



Dhana hii kama ilivyoanzishwa na mahakama katika shauri la Denise dhidi ya Denise, Jaji Single anasisitiza kwamba dhana hii ni ngumu kuipinga isipokuwa kama itathibitika kwamba mwanaume aliyekutwa ni hanithi au mwanamke huyo ni bikira.



Na uthibitisho wa uzinifu nje ya ndoa ni kama uthibitisho wa katika kesi ya jinai ambapo anayelalamika anatakiwa kuithibitishia mahakama pasi na shaka kwamba uzinifu umetokea.
Kwa upande wa Uingereza, kama itathibitika kwamba kulikuwa na uzinifu na kwamba mtoto alizaliwa nje ya ndoa, pia atahesabika ni mtoto haramu na hivyo kukosa haki zake zote kwa mzazi wake wa pili.
Hata hivyo, mara nyingi uzinifu unaweza kuthibitishwa na ushahidi wa mazingira kama vile mmoja wa wanandoa kuwa na ugonjwa wa zinaa na kadhalika.



Kifungu cha 170(2) cha sheria ya ndoa ya Tanzania, kinatoa maelekezo juu ya ushahidi wa aina hii.
Hata hivyo, uzinifu si lazima uwe sababu ya mahakama kutoa talaka. Mahakama kwa kuzingatia mazingira ya kesi husika inaweza kuamuru mtu aliyefanya uzinifu na mmoja wa wanandoa kumlipa fidia muathirika wa uzinifu huo.



Ukatili pia ni sababu mojawapo ya sababu zinazoweza kuithibitishia mahakama kwamba ndoa hii ina kasoro zisizoweza kurekebishika.



Kuharamisha, kubatilisha ndoa katika Sheria ya Ndoa

NENO kuharamisha ni la kawaida katika lugha ya Kiswahili ambalo linalotokana na neno ‘haramu’ likimaanisha kitu kisichofaa, kwa maana iliyo nyepesi.
Aidha kuharamisha ndoa kisheria ni kitendo cha mahakama kutoa tamko kwamba ndoa ambayo iliyodhaniwa kuwa imefungwa haikufungwa wala haikuwapo.



Hapa tunatakiwa tujue mantiki ya kitendo hiki ni kuharamisha (nullify) ndoa ambayo ilidhaniwa ni halali wakati wa kufungwa, lakini kumbe katika jicho la sheria ndoa hiyo “haipo na wala haikuwahi kuwapo”.



Hii siyo talaka kama ambavyo watu wengine wanaweza kufikiri. Somo la talaka tutalizungumzia baadae katika makala nyingine.



Kama ambavyo nadharia nyingi za sheria zetu zimetoka katika sheria za mahakama za nchini Uingereza, yaani Common law, nadharia hii imetoka huko huko, wakati wa mageuzi baada ya kuanguka kwa dola ya utawala wa kifalme wa Kirumi huko Ulaya.



Wakati wa utawala wa kirumi huko Ulaya, sheria za Kanisa Katoliki zilikuwa zinatumika kwa kiwango kikubwa, imani na mafundisho ya Kanisa Katoliki ndoa ni Sakramenti iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu.



Hii ilikuwa na maana kuwa ndoa ni takatifu hivyo talaka ni kitu ambacho hakitambuliki katika sheria za Kanisa, kusisitiza maneno ya bwana Yesu katika Injili ya Marko 10:7-8 kwamba mwanaume na mwanamke wakiungana wanakuwa mwili mmoja na kwamba alichokiunganisha Mungu mwanadamu yeyote asikitenganishe.



Kwa mantiki hiyo, njia pekee ya watu kutoka ndani ya ndoa wakati huo ilikuwa ni kuiharamisha na si talaka, kwani ilikuwa haitambuliki kama tulivyoona hapo awali. Baada ya kuanguka kwa dola ya Rumi huko Ulaya, tawala za kifalme zikawa maarufu sehemu nyingi huko Ulaya na kusababisha sheria za kanisa (Canon law) kupotea na kwa upande wa Uingereza, sheria za mahakama za Uingereza yaani Common law zikashika kasi.



Hivyo basi athari ya sheria hizi za mahakama za Uingereza ilikuwa ni pamoja na kuleta mafundisho mengine ikiwemo kuanzisha upya talaka.
Kwa Tanzania, vifungu vya 39 na 49 vya Sheria ya Ndoa, 1971; vinaelezea njia mbili kuu za kuharamisha ndoa. Njia hizi ni zile ambazo ikithibitika mahakamani, basi mahakama itatoa tamko la kuharamisha ndoa.



Njia hizi ni pamoja na ndoa haramu (void marriage) na ndoa isiyo haramu lakini pia si halali kwa kuwa imekosa mahitaji kadhaa ya kisheria yaani ndoa batili ( voidable marriage).
Kwa ndoa haramu, hii ni ndoa ambayo tangu mwanzo ilikuwa ni haramu katika jicho la sheria; wakati aina ya pili ya ndoa isiyo haramu ila imekosa kutimiza masharti kadhaa ya kisheria kuifanya iwe halali na hivyo kuifanya batili.



Kwa mfano kwa mwanamme asieweza kufanya tendo la ndoa na mkewe, ndoa yake itakuwa batili kama mkewe atakwenda mahakamani kuomba ndoa yake ibatilishwe kwa kuwa mumewe hawezi kufanya tendo hilo ambalo ni hitaji la kisheria ili ndoa iwe halali; lakini kama mwanamke huyo atavumilia hali hiyo, ndoa yao itakuwa ni halali.



Hivyo basi, kwa mujibu wa kifungu cha 39 na 49 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha ndoa isiwe halali, kwa sababu hizo mume au mke anaweza kuomba mahakama itoe tamko la kubatilisha ndoa yake. Sababu hizi ni kama zifuatavyo;
Kwanza, kwa wanandoa kushindwa kufanya tendo la ndoa wakati wameoana, kwa mujibu wa kifungu cha 39(e) cha Sheria hii, pindi mwanandoa yeyote (mwanamme au mwanamke) wakati wameshafunga ndoa na mwenzake atashindwa kufanya tendo la ndoa hiyo itakuwa sababu kwa mmojawapo kuomba tamko la kubatilisha ndoa hiyo.



Huu pia ni uamuzi uliotolewa katika shauri la Dralge dhidi ya Dralge , (1947)1 All.ER 29), la nchini Uingereza,ambapo mahakama ilitafsiri kimantiki kwamba tendo la ndoa ndilo haswa linalomaanishwa katika kile ambacho kifungu cha 39 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inamaanisha.

No comments: