JAJI MKUU WA TANZANIA MHE. MOHAMED CHANDE OTHMAN AMSHUKURU RAIS MHE. DKT. JOHN POMBE MAGUFULI KWA KUTIMIZA AHADI YAKE.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia Mahakama kiasi cha shilingi Bilioni 12.3. zitakazotumika  katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama na ujenzi wa Mahakama mpya katika maeneo mbalimbali nchini. Kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto).
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe (wa pili kutoka kushoto) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu Serikali kuendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuwezesha ufanisi wa shughuli zake.
……………………………………………………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia Mahakama kiasi cha shilingi Bilioni 12.3 alizoahidi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, 2016 jijini Dar es salaam.
Amesema Fedha hizo zitatumika  katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama na ujenzi wa Mahakama mpya katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa shukrani hizo leo jijini Dar es salaam Mhe.Othman amesema kuwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 Mahakama imepata asilimia 100 ya fedha zote za Maendeleo zilizokasimiwa na Bunge kwenye Bajeti yake ya mwaka 2015/2016.
Amesema  kupatikana kwa fedha hizo ambazo ni za Maendeleo kutasaidia kufufua miradi ya ujenzi iliyosimama, kufufua Mahakama ambazo zilikua hazifanyi kazi kwa sababu ya uchakavu na kuipatia Mahakama fursa zaidi ya kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwasogezea huduma za Haki karibu katika maeneo wanayoishi.
Mhe.Othman ameeleza kuwa kwa kipindi cha bajeti za miaka 3 mfululizo kuanzia mwaka 2012 /2013 hadi 2014/2015  Mahakama ilikua ikipokea fedha pungufu ya kiasi kilichopangwa katika Bajeti hali iliyochangia kuzorota kwa shughuli za Mahakama.
” Kwa mara ya kwanza Mahakama tumepata asilimia 100 ya Bajeti yetu ya mwaka 2015/2016 kutoaka Serikalini, mwaka 2012/2013 tulipata shilingi bilioni 26.9 ikiwa ni pungufu ya bajeti yetu kwa asilimia 78, mwaka 2013/2014 tukapata Bilioni 42.7 pungufu kwa asilimia 82 na mwaka 2014/2015 tulipewa shilingi  bilioni 41.5 ambayo ni pungufu kwa asilimia 92 “
Akizungumzia miradi ya ujenzi wa majengo mapya ya Mahakama amesema kuwa tayari Mahakama ina michoro ya ramani za majengo yatakayojengwa katika maeneo mbalimbali ambayo hayakuwa na huduma hiyo ikiwemo mikoa 12 kati ya 25 ambayo haina Mahakama Kuu, wilaya 22 kati ya 133 ambazo hazina Mahakama za Wilaya pamoja na kuongeza Mahakama za Mwanzo ambazo ziko 976 kufikia kata zote 3,957.
Kuhusu  Mradi wa ujenzi wa  jengo la Makao Makuu ya Mahakama utakaofanyika katika uwanja wa Chimala jijini Dar es salaam amesema  utahusisha  maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za Kimahakama na kuongeza kuwa  Mahakama itajenga  jengo lenye viwango kwa kuwatumia Wakandarasi  na wataalam wa kitanzania watakaojenga  Mahakama nzuri na yenye viwango kwa gharama  nafuu.
“Mahakama tutatoa kipaumbele kwa wataalam wetu wa ndani ili waweze kutujengea Mahakama zetu, tunalenga kuwafikishia huduma zetu katika maeneo wanayoishi  tunao mfano mzuri wa Mahakama ya mwanzo ya Dumila iliyoko Morogoro, Mahakama hii imejengwa kijijini ni ya kisasa” Amesisitiza Mhe.Othman.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaendelea  kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuwezesha ufanisi wa shughuli zake kwa kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha za Bajeti kinachopitishwa kwa ajili ya kuhudumia shughuli za  Mahakama kinafika kwa wakati.
Akizungumzia kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, amesema uanzishwaji wake uko katika hatua nzuri na wakati ukifika wananchi watataarifiwa kama ilivyoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuungwa mkono na Mahakama ya Tanzania.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip  Mpango, akizungumzia fedha za Maendeleo zilizotolewa  na Mhe.Rais amesema kuwa lengo la ahadi ya Rais kwa Mahakama ilikua ni kuhakikisha Haki inapatikana kwa wananchi kwa Wakati na kwamba miongoni mwa vitu vilivyokua vikichelewesha haki kwa watanzania walio na mashauri Mahakamani ni ukosefu wa fedha na uchakavu wa miundombinu.
Amesema Serikali inaendelea kujenga uwezo wa kifedha ili kuimarisha huduma katika mihimili yote ikiwemo Bunge na Mahakama huku msisitizo ukiwekwa katika kukusanya mapato ya ndani.
“Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tuna dhamira ya dhati ya kukusanya mapato ya ndani ili kujenga uwezo wa Serikali tutawabana wote waliokuwa wanakwepa kulipa kodi na hili tutalisimamia kikamilifu”
Amesema utoaji wa Haki ni moja ya ukuzaji wa maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa Mahakama ya Tanzania inafanya kazi nzuri pamoja na ufinyu wa bajeti yake.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.