Thursday, March 10, 2016

ACT WAZALENDO watoa kauli kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti Mhe. Truong Tan Sang

vie3Chama cha ACT Wazalendo kinaipa uzito wa kipekee ziara ya kwanza nchini na barani Afrika ya rais wa taifa la Kisoshalisti la Vietnam Truong Sang anayezuru Tanzania kuanzia siku ya Jumatano tarehe 9 Machi, 2016.
Kwetu Chama cha Wazalendo, Vietnam ni mfano wa kuigwa na nchi zinazoendelea juu ya umuhimu wa sera bora na usimamizi thabiti wa rasilimali katika kuipaisha nchi kiuchumi.
Tanzania na Vietnam zilipopata uhuru, zilikuwa katika kiwango kinachokaribiana kiuchumi. Sasa Vietnam imesonga mbele kiuchumi mara dufu zaidi ya Tanzania karibu kwenye kila nyanja. 

Mifano ni mingi: Vietnam iliyokuja kuchukua mbegu na kujifunza upandaji wa mikorosho nchini Tanzania ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa korosho ghafi kwa sasa. Tofauti na Tanzania ambayo huuza sehemu kubwa ya korosho zake zikiwa ghafi, nchini Vietnam korosho hubanguliwa kabla ya kuuzwa ndani na nje ya nchi ili kuziongezea thamani.
Haya yamewezekana kwa sababu, pamoja na mambo mengine, Vietnam imewekeza katika uendelezaji wa teknolojia rahisi ya ubanguaji wa korosho vijijini ambapo korosho zinabanguliwa vijijini zinakozalishwa na kuongeza ajira.

Pia, Vietnam iliyokuja kuchukua mbegu ya kahawa Tanzania ndiyo nchi ya pili kwa uzalishaji wa kahawa duniani kwa sasa ikitanguliwa na Brazil. Vietnam imewahi pia kuchukua samaki aina ya Sato ili kuendeleza sekta yao ya uvuvi. Swali la kujiuliza, sisi tunachukua nini kutoka Vietnam?

Vietnam inafanya vyema zaidi pia kwenye maeneo ya viwanda, usalama wa chakula, teknolojia ya mawasiliano na ustawi wa watu wake.

Wakati Tanzania ikikumbatia masharti ya soko huria na kubinafsisha kiholela viwanda, mashamba ya umma na makampuni kwa maelekezo ya mashirika ya fedha ya kimataifa, Vietnam ilibuni mfumo wake wa mageuzi ya kiuchumi (“Doi Moi”) unaovutia mitaji binafsi ili ishindane na mitaji ya dola.
Maono na msimamo wa kiuchumi wa ACT Wazalendo daima umekuwa ni ujenzi wa uchumi unaostawisha sekta binafsi bila kuathiri jukumu la dola kuhodhi sekta nyeti za kiuchumi kwa manufaa ya umma.

Ziara ya Rais wa Taifa la kijamaa la Vietnam ifumbue macho serikali ya CCM kutoka kwenye maneno matupu ya uchumi wa viwanda na kwenda kwenye vitendo. Mawaziri wa CCM wamekuwa wakiendelea kutoa ahadi za ujenzi wa viwanda kana kwamba bado tupo kwenye kampeni. Chama cha ACT kinawashawishi wananchi kuhitaji utekelezaji wa ahadi sasa.
Tunachukua fursa hii kukukaribisha sana Tanzania Rais Truong Sang.

Imetolewa leo tarehe 9, Machi 2016.
Ado Shaibu,
Katibu, Itikadi, Mawasiliano kwa Umma na Uenezi.
Simu: 0653619906

No comments: