Monday, March 21, 2016

Alipoulizwa nini hatma ya Z'bar baada ya uchaguzi jana,Maalim Seif amesema..


Alipoulizwa nini hatma ya Zanzibar baada ya uchaguzi wa marudio uliofanyika jana, Maalim Seif amesema yeye hajui ila waulizwe CCM maana wao ndio wanajua wamekusudia nini na wanapeleka wapi nchi hii.

 
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinasaka kura za kumpa ushindi mgombea wao wa urais Zanzibar mithili ya msako wa ngedere.Akizungumza katika Hoteli ya Serena jana, ambako yupo kwa mapumziko ya matibabu, Maalim Seif alisema CCM inataka kushika madaraka kwa kutumia kila aina ya nguvu.

Alisema kinachofanyika Zanzibar si uchaguzi bali ni kumtangaza Rais Dk. Mohamed Ali Shein kuwa rais wa Zanzibar baada ya kufuta matokeo halali ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ambayo yalimpa ushindi.Alisema ili kutimiza azma ya kumtangaza Dk. Shein, CCM wamelazimika kutafuta kura kwa kuwabana watumishi wote nje ya Zanzibar kurudi visiwani humo kupiga kura na kwamba anayekaidi agizo atakuwa amejifukuzisha kazi

 mwenyewe.“Kinachofanyika si uchaguzi, bali ni kumtangaza Dk. Shein kuwa rais…CCM wanasaka kura utafikiri wanasaka ngedere porini…watumishi wote waliopo nje ya Zanzibar wamelazimishwa kurudi wapige kura.“Sasa tunasubiri tu Rais atangazwe na kuapishwa. Hata wakimtangaza Dk. Shein mshindi atakuwa ni Rais wa Jecha (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha) na CCM.“Ukweli ni kwamba Wazanzibari wanajua rais wa mioyo yao, ni Maalim Seif na hawawezi kufuta hilo,”alisema.

Alisema anasikitika Zanzibar kurudi katika siasa za uhasama na chuki ambazo walizimaliza mwaka 2010 baada ya kuwa na maridhiano na kuunda serikali ya umoja wa taifa.“Mimi nasikitika CCM imeturudisha nyuma kwenye siasa za uhasama, chuki na uonevu. Mwaka 2010 tulifanya maridhiano mazuri tukamaliza haya mambo, sasa yamejirudia… hali ni mbaya wakuulizwa hatma ya Zanzibar ni CCM kwa sababu wao ndiyo wameamua tuwe hapa tulipo,” alisema. 

No comments: