TAARIFA KWA UMMA JUU YA UAMUZI WA SPIKA KUWABADILISHIA KAMATI WABUNGE WALIOTUHUMIWA KWA RUSHWA

https://2.bp.blogspot.com/-dLjEAPPBUdc/VvKRN5YsV-I/AAAAAAAIeqo/PWgJOLS950M0EAp1pd6ekes810xno7gXg/s1600/1.JPG
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa, wa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Chama cha ACT Wazalendo wakimtaka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda mara moja kamati ya uchunguzi kwa kamati zote zilizotuhumiwa ili ukweli ubainike na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.


 CHAMAACT- cha Wazalendo imepokea kwa masikitiko uamuzi uliofanywa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Job Ndugai, kuwahamisha kamati Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Wajumbe wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge uliofanywa jana tarehe 22.3.2016.
Ikumbukwe kuwa uamuzi huu wa spika unafuatia kashfa nzito ya viongozi na wajumbe wa kamati mbalimbali za Bunge kupokea rushwa kutoka mashirika tofauti ya  umma kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari

Kufuatia taarifa hiyo ya inayoiaibisha mhimili huo wenye jukumu la kuisimamia serikali , baadhi ya wabunge akiwemo Ndugu Zitto Ruyagwa Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama chetu cha ACT Wazalendo walimwandikia barua za kujiuzulu Mh. Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano ili kupisha uchunguzi ufanyike na wataobainika kupokea rushwa kuchukuliwa hatua za kisheria.


Chama chetu kinampongeza Mbunge wetu na Wabunge wengine waliochukua hatua ya kujiuzulu ujumbe kwenye kamati zao ili kupisha uchunguzi. Uamuzi huo wa ndugu Zitto unakwenda  sambamba na misingi ya Chama chetu cha ACT Wazalendo ya uadilifu na uwajibikaji.

Tangu mabunge yaliyopita, kamati za Bunge zimekuwa zikituhumiwa mara kadhaa kujihusha na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa Mashirika ya Umma, Makampuni na watu binafsi. Rai iliyotolewa mara kwa mara huko nyuma ya kuitishwa kwa uchunguzi ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge ilipuuzwa na  matokeo yake, kashfa hizi zimeliondolea heshima Bunge na Wabunge.

Kwa mujibu wa Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge ndiyo chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. Kinapotuhumiwa kupokea rushwa, kinawezaje chenyewe kuisimamia serikali na kuongoza mapambano dhidi ya rushwa?

Uamuzi wa kuwahamisha Kamati viongozi na wajumbe wa Kamati zilizotuhumiwa kupokea rushwa ni sawa na kuufunika uozo na kuendeleza utamaduni mbovu wa siku nyingi hapa nchini wa kuwahamisha au “kuwapangia kazi nyingine” viongozi na watumishi wa umma wanaotuhumiwa kupokea rushwa au kukosa ufanisi. Kimsingi Utamaduni huu unafifisha mapambano dhidi ya rushwa na uwajibikaji.

Chama cha ACT Wazalendo kinamtaka Spika wa Bunge la Jamhuri wa Tanzania kuitisha mara moja uchunguzi kwa kamati zote zilizotuhumiwa ili ukweli ubainike na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja,kuwahamisha kamati Wabunge kamwe hakutaondoa tatizo na kulirejeshea Bunge hadhi yake.
Tunamtaka Mh. Spika kuonyesha kwa vitendo jinsi ofisi yake inavyochukizwa na vitendo vya rushwa nchini kwa kuitisha uchunguzi utaovishirikisha vyombo vya dola ili ukweli ujulikane.

Ndugu Yeremia Kulwa Maganja,
Mwenyekiti, Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa,
ACT Wazalendo
23/03/2016

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.