Monday, March 21, 2016

TAIFA STARS YAWASILI D'JAMENA


Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kundi la kwanza limewasili salama jijini D’jamena nchini Chad tayari kwa mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017.

Taifa Stars inayonolewa na kocha mkuu Charles Boniface Mkwasa akisaidiwa na Hemed Morocco kimewasili D’jamena leo majira ya saa 7 mchana kwa saa za huku kwa shirika la ndege la Ethiopia, sawa na saa saa 9 alasiri kwa saa za nyumbani na Afrika Mashariki na kufikia katika hoteli ya Legder Plaza.
Msafara wa 20 wa kundi la kwanza uliowasili umejumuisha viongozi pamoja na wachezaji 12, huku kundi la pili likitarajiwa kuondoka Tanzania Jumatatu usiku na kuwasili Jumanne kuungana kwa mazoezi ya mwisho nchini humu.
Stars inatarajiwa kufanya mazoezi kesho Jumatatu na Jumanne katika uwanja wa Omnisports Idrissm Mahamat Ouya kujiandaa na mchezo huo wa Jumatano katika dimba hilo hilo jijini D’jamena.
Wachezaji waliowasili nchini ni Chad ni Ally Mustafa, Juma Abdul, Haji Mwinyi, kelvin Yondani, Deus Kaseke, Mohamed Hussein, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim na nahodha Mbwana Samatta.
Mchezo kati ya Chad dhidi ya Tanzania unatarajiwa kuchezwa siku ya Jumatano Alasiri kwa saa za huku, sawa na saa 11 jioni kwa saa za nyumbani Tanzania.

No comments: