Wednesday, March 23, 2016

TRA na JICA kutoa mafunzo ya ukusanyaji kodi awamu ya pili


tr1
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Victor Kimaro (katikati) akizungumza na  waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam kuhusu  kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa kuwajengea uwezo wa kitaalam watumishi wa mamlaka hiyo ili kuongeza makusanyo ya ndani , kushoto ni mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) Toshio Nagase na kulia ni Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo.
tr2
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) Toshio Nagase (kushoto) akizungumza na  waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam kuhusu  kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa kuwajengea uwezo wa kitaalam watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mkakati wa kuanza kwa awamu ya pili ya mradi huo, katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali TRA Bw. Victor Kimaro na kulia ni Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo.

………………………………………………………………………………………………………………………
Na. Eliphace Marwa-Maelezo
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamekamilisha awamu ya kwanza ya kutoa mafunzo ya kuwajenga uwezo wafanyakazi wake ili kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko ya ukusanyaji kodi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka hiyo Bw. Victor Kimaro amesema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa ushirikiano wa TRA na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa muda wa miaka minne tangu Februari 2012 hadi Machi 2016.
Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TRA ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya ukusanyaji wa kodi ambapo wataalam toka JICA wameweza kuwajengea uwezo wa kitaalam wa kuboresha makusanyo ya ndani.

“Kwa sasa wafanyakazi hawa wataweza kuboresha mazingira ya ulipaji kodi ambayo huwa yanabadilika kutokana na baadhi ya watu kukwepa kodi” alisema Bw. Kimaro..
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Kodi Profesa Isaya Jairo amesema kuwa jumla ya wafanyakazi 608 wa Mamlaka hiyo wamefaidika na mafunzo hayo ambayo yamegharimu zaidi ya dola za kimarekani milioni 3.5.

“Kwa sasa baada ya kukamilika kwa mafunzo haya ya awamu ya kwanza, mamlaka itaweza kuongeza makusanyo ya mapato kutokana na uwezo wa kiutaalam walioupata watumishi wa TRA” alisema Prof. Jairo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA, Bw. Toshio Nagase, alisema Serikali ya Japan imekubali kuanza mradi mwingine wa ushirikiano wa kitaalam kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ili kuendeleza ushirikiano kati ya TRA na JICA.

Awamu ya pili ya mafunzo ya kujenga uwezo wa kitaalam yanatarajiwa kuanza mwaka huu mara baada ya Makao Makuu ya Shirika la Maendeleo la Japan kumaliza kufanya uchambuzi wa maandalizi na kuchagua mbinu za utekelezaji wa mradi huo.

No comments: