Monday, May 9, 2016

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAENDELEA KUPUNGUA.

V1Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akita taarifa ya kuongezeka kidogo kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Aprili 2016 leo jijini Dar es salaam, Kulia ni Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji Semboja.Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Aprili 2016 umepungua hadi asilimia  5.1  kutoka asilimia 5.4.
V2Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji Semboja akifafanua kwa waandishi wa Habari kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania.
V3Waandishi wa Habari wakiwa kazini, wakati Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikitangaza Mfumuko wa Bei Mwezi Aprili 2016 leo jijini Dar es salaam.
……………………………………………………………..


Na. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)  Dar es salaam.
 
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Aprili 2016 na kusema kuwa umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.4 iliyokuwepo mwezi Machi, 2016.
Hii inamaanisha kuwa  kasi ya upandaji wa bei ya  bidhaa na huduma kwa mwezi Aprili 2016 imepungua kidogo ikilinganishwa na kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma  iliyokuwepo mwezi Machi mwaka huu.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo ametoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam na kueleza kuwa kupungua kwa mfumuko huo kumesababishwa na kupungua kwa kasi ya bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Takwimu zilizokusanywa katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwenye bidhaa zinazotumika kupima mfumuko wa bei kwa mwezi Aprili 2016 zimeainisha kuwa bidhaa zisizo za vyakula katika soko zikiwemo Gesi , dizeli na mafuta ya taa zimechangia kupungua kwa mfumuko huo.

Amesema kuwa pamoja na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa hizo kwa mwezi Aprili 2016, baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mchele, unga wa Mahindi na mkaa ilionyesha kuongezeka katika kipindi hicho.
Akizungumzia Kuhusu Fahirisi za Bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi hapa Tanzania kwa mwezi Machi na Aprili Bw. Kwesigabo amesema kuwa zimeongezeka hadi kufikia 102.46 kutoka 101:93 za mwezi Aprili.

Amesema kuwa tofauti na mwezi Machi bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi kwa mwezi Aprili ni unga wa muhogo, dagaa, choroko, maziwa ya ungana na matunda aina ya machungwa.
Aidha,bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na mvinyo, bia kuni na mazulia.

Kwa upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Aprili, 2016 umefikia shilingi 97 na senti 60 ikilinganishwa na uwezo wa shilingi 98 na senti 11  wa mwezi Machi 2016.
“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Aprili 2016 umepungua, hii ina maana kuwa sasa mtu anahitaji kuongeza  ya shilingi 2.40 ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa na zile alizokuwa na uwezo wa kuzinunua mwezi Machi ” Amesema Kwesigabo.

Kwa upande wa mfumuko wa Bei kwa nchi za Afrika Mashariki mwezi Machi, 2016, Kwesigabo amesema una mwelekeo unaofanana; Kenya umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 5.27 kutoka 6.45 huku Uganda ukifikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 6.2 zIlizokuwepo mwezi Machi 2016

No comments: