MREMA AMSHUKIA MAALIM SEIF
Na Mwandishi wetu
MWENYEKITI Taifa wa Chama cha TLP, Augustino Mrema,amemshukia Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff, kuwa kauli zake anazotoa zinaweza kuvunjika kwa amani nchini.

Hata hivyo amelishangaa jeshi la polisi kutomkamata kiongozi huyo kwa kutoa kauli ambazo hazina tofauti na uhaini.

Mrema ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuzungumzia hali ya amani visiwani Zanzibar.

“Tunaona Maalim Seif amedekezwa na endapo ataendelea na uchochezi wake hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu zichukuliwe dhidi yake, tunaamini hayupo juu ya Katiba na sheria za nchi,”alisema Mrema huku akinukuu kauli alizodai zilishawahi kutolewa na maalim Seif.

Mrema alinukuu baadhi ya kauli hizo kuwa ni Maalim Seif kudai kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohamed Shein hatamaliza miaka mitano madarakani, kujitangazia matokeo ya uchaguzi kinyume cha sheria na kudai kuwafungulia mashtaka viongozi katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
Mrema ambaye alishawahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, alisema wazanzibar wajihadhari na kauli za mwanasiasa huyo na wasiruhusu amani ya nchi ivurugike kwani amani ya Zanzibar ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya mtu binafsi.

Alisema amani ya Zanzibar ikivurugika hata Tanzania Bara itaathirika. Pia wananchi wote kwa ujumla wataathirika bila kujali kwamba ni wafuasi wa CUF, CCM au CHADEMA.
Alisema maalim Seif atambue kuwa siyo lazima awe Rais wa Zanzibar ndipo nchi itulie kwani kuna njia nyingi za kutafuta haki na siyo kufanya maandamano ambayo wanaoathirika ni watu wa kawaida na wengine kupoteza maisha kama ilivyotokea mwaka 2001.

“Badala ya Maalim Seif kudai kwamba viongozi wa Serikali wapelekwe ICC kwa yale mauaji ya 2001, yeye ndiye aliyepaswa kupelekwa kutokana na kuwachochea wananchi wafanye maandamano haramu, pia ICC siyo kwamba wanapelekwa viongozi wa serikali tu hata wa upinzani wakisababisha mauaji ya halaiki,”alisema.

Mrema akizungumzia marudio ya uchaguzi wa Zanzibara uliofanyika Machi 20, mwaka huu, alisema hatua ya CUF kususia uchaguzi huo siyo kujenga chama bali ni hatari kwa mstakabari wa chama ambacho kinaweza kusambaratika.
Alitoa mfano Chama cha UNIP cha Zambia kilichokuwa kikiongozwa na Dk. Keneth Kaunda na Chama cha UPC cha Uganda kilichokuwa kikiongozwa na hayati Dk.Milton Obote vilisambaratika kutokana na kususia uchaguzi mkuu wan chi hizo.

Mrema alisema kujitangazia matokeo Maalim Seif lilikuwa ni kosa la jinai kwa kuvunja Katiba ya Zanzibar na alistahili kuchukuliwa hatua lakini cha kushangaza hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake.

“Kiongozi wa upinzani Uganda Dk.Kiiza Besigye alishtakiwa baada ya kujitangaza mwenyewe kushinda na kujiapisha kuwa rais, lakini hapa kwetu maalim Seif hajachukuliwa hatua yeyote, anadekezwa, sijui wanamuogopa,”alisema.

Kuhusu kuhamasisha wafadhili kusitisha misaada Tanzania kwa sababu ya uchaguzi Zanzibar, kufanya hivyo siyo jambo zuri kwa sababu watakaoathirika ni wananchi watakaokosa huduma na pia ni kuingia mambo ya ndani ya nchi.
MWISHO

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.