Thursday, June 23, 2016

MICHEZONI LEO KUTOKA TFF


MCHEZO YOUNG AFRICANS, TP MAZEMBE


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limekataa ombi la Young Africans ya Dar es Salaam juu ya kubadili siku na muda wa mchezo dhidi ya T.P. Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika taarifa ya CAF iliyofika TFF imesema mchezo huo utafanyika Jumanne Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kama ulivyopangwa awali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Young Africans kwa upande wao waliomba mchezo huo ufanyike Juni 29, 2016 saa 1.30 usiku.
Kadhalika, kikao cha maandalizi katika mchezo huo kiliochofanyika leo Juni 23, 2016 kimeagiza uongozi wa Young Africans kuwaelimisha mashabiki wao kukaa katika eneo la mazoea tofauti na mipango yao ya kutaka kukaa eneo lote la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africans ya Dar es Salaam, Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), utachezeshwa na Mwamuzi Janny Sikazwe wa Zambia.

Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba. Kamishna wa mchezo huo atakuwa Celestin Ntangungira wa Rwanda. Pia mchezo huo utakuwa na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.


…………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA

Timu ya soka ya Vijana ya Shelisheli, inatarajiwa kuingia Dar es Salaam, Tanzania kesho saa 7.45 usiku (usiku wa kuamkia Ijumaa Juni 24, 2016), kwa ajili ya mchezo dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ utakaofanyika Juni 26, 2016 kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo inaingia wachezaji na pamoja na viongozi 25 ka ujumla wake na itafikia hoteli ya Southern Sun iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Waamuzi wanne kutoka Ethiopia, ndio watakaochezesha mchezo wa kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na Shelisheli utakaofanyika Juni 26, 2016 kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17. Waamuzi hao ni Belay Tadesse Asserese ambaye ni mwamuzi wa kati wakati wasaidizi wake ni Tigle Gizaw Belachew upande wa kulia na Kinfe Yilma Kinfe upande wa kushoto huku mwamuzi wa akiba atakuwa Lemma Nigussie. Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Bester Kalombo.

Serengeti Boys ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mchezo huo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana wenzao wa Shelisheli utakaofanyika Juni 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Mchezo wa marudiano kati ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.

Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.


No comments: