Thursday, June 23, 2016

SHEIKH JALALA AWAPA NENO WANAODHANI KUWA WALEMAVU WA NGOZI (ALBINO) WANALETA UTAJIRI


Sehemu ya walemavu wa ngozi waliohudhuria Iftari katika msikiti wa Al GhadirKigogo, wakifuatilia kwa makini hutba iliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa dhehebu la Shia Ithnasheria Sheikh Hemed Jalala.
Sheikh Hemed Jalala akizungumza katika Iftari hiyo. Msikiti wa Al Ghadir  Kigogo umewaalika watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwa ni ishara ya kuonyesha kwa umma kuwa hao nao ni binadamu kama walivyo wengine na wanahitaji kupata haki sawa kama wengine.





Kiongozi Mkuu wa Waislamu dhehebu la shia Ithnasheria amewataka jamii kufahamu kuwa hakuna njia ya mkato ya kupata utajiri na kwamba wale wote ambao wanaamini katika kuua watu wenye ulemavu wa ngozi ili wanufaike wanapaswa kuacha tabia hiyo kwani ni kwenda kinyume na mufundisho ya dini zote duniani.

Akizungumza katika iftari maalum na watu wenye ulemavu wa ngozi kutoka Wilaya ya Kinondoni, Sheikh Jalala amesema viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kulizungumza hilo bila woga kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi.

Amesema Albino ni binadamu kama walivyo watu wengine hapa nchini, wanahaki sawa ya kuishi, kulindwa na nyinginezo hivyo si haki kukatiza maisha ya watu hao na kwamba dini zote za duniani haziruhusu watu kuuana.

Aidha sheikh Jalala amefafanua njia nzuri za kupata utajiri kuwa ni kufanya kazi kwa bidii zote na si kuwaza Imaani potofu ya kuua watu wengine ambao hawana hatia.
Amesema kitendo cha kuua kinazima ndoto zao, hivyo ni wakati watu wakafahamu hilo na kuachana na tabia hiyo ambayo inatia doa Taifa la Tanzania huko Ulimwenguni.

“Nataka niseme, tendo la kuwaita wenzetu wenye ulemavu wa ngozi na kushiriki pamoja futari ya jioni hii ni kuonyesha kuwa hawa ni wenzetu, hawana utofauti wowote na wengine, wanahaki sawa kama Watanzania…kuwaua ni matendo ya kishetani na hayakubariki” alisema Sheikh Jalala
Amesema wale wote ambao bado wana Imaani ya kuua ili watajirike ni washamba na hawajui walifanyalo, wanapaswa kufahamu kuwa utajiri hauletwi kwa damu za watu badala yake ni kujituma kwa kufanya kazi inayompendeza Mungu.

Katika hatua nyingine Sheikh Jalala amewaahidi chama cha watu wenye ulemavu wa Ngozi Wilaya ya Kinondoni kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji na kwamba wanakaribishwa katika msikiti wa Kigogo muda wowote na watapewa ushirikiano unaostahili.

“Nataka niwaambie ndugu zangu wenye ulemavu wa ngozi hapa Tanzania sisi hapa Kigogo tunawapenda na tunawakaribisha hapa msikitini ,sisi hatujui kubaguana,muone kama mko nyumbani na kwamba muda wowote mkiwa na haja ya kutuona milango iko wazi na mnakaribishwa sana ”Alisema Sheikh Jalala.

Akizungumzia Msikiti wa Kigogo Sheikh Jalala amesema ni kimbilio la watu wote, ni msikiti wa wakristo, watu wenye ulemavu wa ngozi, wajane na masikini. Ni msikiti ambao unajari imaani za watu tofauti kwani wanaamini kuwa haitokea siku moja nchi yote ya Tanzania kukawa na dini moja hivyo si wakati wa kubaguwana.

Haitakaa itokee Tanzania kukawa na dini moja mpaka dunia inapogota mwisho wake…lakini mtakubaliana na mimi kuwa Mungu aliyeumba Mkiristu ndiyo huyo aliyemuumba muislamu na wale wa Dini nyingine, Mwanzo wa binadamu ni uleule wa Adamu na hawa…tofauti zilizopo ni za kibinadamu hatuna haja ya kubaguana.Alisema.

Ametoa wito kwa Watanzania kupinga mauaji ya Albino kwa vitendo na kuwataka viongozi wa dini kutumia membari zao kukemea viitendo viovu vya mauaji ya albino.

No comments: