Wednesday, June 22, 2016

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO WAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA OFISINI HAZINA.

1Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Gideon Manambo akizungumza na watumishi wa Wizara (hawapo pichani) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Bw. Doto James.
2Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakifurahia jambo wakati Mwenyekiti wa mkutano  huo  ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Bw. Doto James akifafanua hoja mbalimbali za  watumishi.
3Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa wamesimama kwa dakika chache kuwakumbuka watumishi waliotangulia mbele za haki kwa mwaka huu, katika mkutano huo.
4Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakibadilishana mawazo baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
6Picha ya pamoja.
——————————————————————-

Wizara ya Fedha na Mipango imeadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya mkutano na Watumishi wake, lengo likiwa ni kujadili mafanikio na changamoto wanazo kabiliana nazo mahali pa kazi.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.  Doto James aliwataka Watumishi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Magufuli katika  kupambana na masuala ya rushwa, uzembe kazini na Watumishi hewa ambao wamekuwa wakiigharimu Serikali fedha nyingi katika kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema Wizara inajipanga kuhakikisha inaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi hasa kwa wale wenye ulemavu kwa  kuwajengea miundombinu rafiki sehemu za kazi ili  kuongeza ufanisi kazini.
“Wizara pia inafanya vizuri katika masuala ya usawa wa kijinsia kwa kuwa na idadi inayoridhisha ya wanawake hasa katika ngazi za maamuzi, ikiwa ni pamoja na kuwa na Manaibu Katibu Wakuu wawili wanawake” . Alisisitiza James
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Fedha na Mipango,  Bw. Gideon Manambo alisema kuwa, watumishi wanatakiwa kufanya kazi kwa ufanisi na kwa  bidii ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya maendeleo ambayo yanahitaji watendaji wenye weledi wa kutosha ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Kwa upande wa watumishi wa Wizara, wameuomba uongozi kuhakikisha kunakuwepo na vitendea kazi vya kutosha ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa na matokeo chanya ambayo yatasaidia kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.
Maadhimisho hayo yamefanyika kufuatia utaratibu mpya uliowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano ambapo uliagiza Wizara pamoja na Taasisi kuadhimisha Wiki hiyo kwa kutatua matatizo ya watumishi wa Umma pamoja na wananchi kwa ujumla katika maeneo yao ya kazi.
Imetolewa na: Mwaipaja
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano  Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango.

No comments: