Wednesday, July 27, 2016

MAAGIZO KWA KLABU ZA LIGI KUU, LIGI DARAJA LA KWANZA

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine ameziasa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutimiza masharti ya kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi Tanzania kwa Wataalamu wa kigeni wakiwamo makocha, madaktari na wachezaji kabla ya kuingia kandarasi.
 
Masharti hayo ni vibali vya kufanya kazi nchini, visa ya kuishi nchini, vibali vya kucheza mpira wa miguu nchini, vibali vya kufundisha mpira na vibali vya watalaamu wengine kama madaktari na hayo ni kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji na Serikali, lakini wakati huohuo kwa wachezaji nao kukatiwa leseni ya kucheza kutoka TFF.
 
“Mchezaji au mtaalamu ye yote anapokuja nchini na kuanza mazoezi na timu yo yote anachukuliwa yuko kazini. Tusingependa watu wapate usumbufu. Kama Katibu Mkuu nimepata taarifa kutoka mamlaka zinazohusika kuwa nifuatiulie kuwa kuwa sisi ndio waratibu soka nchini, natakiwa kufuatilia,” amesema Selestine.
 
“Vilabu vihakikishe vyeti vya taaluma vinawasilishwa TFF kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kutiliana kandarasi na wachezaji au walimu. Inawezekana hawahitajiki. Ni vema wakafanya uratatibu wa kuhakiki,” amesema.
 
Wakati huohuo, huo huo TFF imeagiza klabu kuendelea na usajili kabla ya Agosti 6, 2016 ambayo itakuwa siku ya mwisho na kwamba hakutakuwa na muda wa kuongezwa kwa klabu ambayo itashindwa kukamilisha usajili kwa wakati.

No comments: